Sisitizo la Putin la kustawishwa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na Russia
-
Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa, uhusiano wa kibiashara na kiuchumi wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni imara, unazidi kutia matumaini na bila ya shaka yoyote mwaka huu, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili, kitaongezeka.
Rais Putin amesema hayo katika hotuba aliyoitoa kwenye Kongamano la Uwekezaji la VTB ambayo ni benki ya pili kwa ukubwa nchini Russia na kuongeza kuwa, hivi sasa kuna miradi muhimu ya kilojistiki, nishati pamoja na ushirikiano wa kiviwanda na kiusalama baina ya Tehran na Moscow na kwamba "koridoo" ya kaskazini-kusini nayo imekaribia kuzinduliwa. Amesema, koridoo hiyo itaongeza mno kiwango cha usafirishaji bidhaa kwa kutumia koridoo hiyo.
Iran na Russia ni nchi jirani ambazo kijadi zina uhusiano mzuri na wa kiistratijia. Ijapokuwa sehemu kubwa ya uhusiano huo imekuwa ikihusiana na masuala ya kisiasa na kiulinzi, lakini kwenye miaka ya hivi karibuni, nchi hizi mbili zimetanua na kutia nguvu uhusiano wao wa kibiashara. Iran na Russia ni miongoni mwa nchi zilizowekewa vikwazo na madola ya kibeberu ya Magharibi, hivyo ushirikiano wa nchi hizi mbili katika masuala ya kiuchumi ni jambo la dharura na ni katika kukamilishana hasa kwa kuzingatia kuwa kustawishwa uhusiano wa kibiashara ni sehemu muhimu ya ufanikishaji wa ushirikiano wa kiuchumi.
Iran na Russia zina mambo chungu nzima ya kuweza kushirikiana na kukamilishana kama vile masuala ya viwandani, ujenzi wa nyumba na miji, sayansi na teknolojia, elimu na maarifa, ufundi na sekta ya vyakula, nishati na njia za mawasiliano na usafirishaji bidhaa. Mambo hayo yanaweza kutumiwa vizuri na kupata mafanikio ya kupigiwa mfano kama ambavyo pia hiyo ni fursa ya kuweza kukabiliana na madola ya kibeberu ya Magharibi ambayo silaha yao kuu dhidi ya nchi huru na zisizokubali kuburuzwa; ni vikwazo vya uchumi.
Inatabiriwa kuwa, baada ya kutiwa saini makubaliano makuu ya ushirikiano wa kimkakati na kistratijia baina ya Tehran na Moscow katika ziara ijayo ya Rais Masoud Pezeshkian huko Russia, kutajitokeza mapinduzi makubwa ya kiuchumi na itaanza awamu mpya ya ushirikiano imara wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili jirani.
Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba kushiriki Iran kwenye taasisi na jumuiya mbalimbali za kieneo, ikiwemo jumuiya ya kiuchumi ya Eurasia ambapo Russia nayo ni mwanachama kwenye jumuiya hiyo, si tu kutapelekea ushirikiano wa kieneo kunawiri na kuimarika zaidi, bali mafanikio ya kimataifa ya Eurasia nayo yataongezeka zaidi na zaidi ikiwa ni nguzo imara ya kiuchumi ulimwenguni.
Alaakullihaal, Russia inaendesha biashara zake kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano za Iran kupitia koridoo ya kaskazini-kusini hadi kwenye bandari za India na hatimaye kuyafikia maji ya kimataifa na kuunganika na ulimwengu mpana wa nje. Wakati huo huo uanachama wa Iran na Russia katika kundi la BRICS pia ni fursa ya kipekee isiyo na mbadala ya kuweza kuwa na mchango mkubwa zaidi kundi hilo katika uchumi wa dunia. Bila ya shaka yoyote mambo hayo yote yana manufaa makubwa si kwa nchi wanachama wa BRICS tu, bali kwa uchumi dunia nzima uchumi ambao utatoka nje ya makucha katili ya madola ya kibeberu ya Magharibi na kila taifa litapata haki zake sawa.
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana rais mteule wa Marekani, Donald Trump akaingiwa na kiwewe kiasi cha kufikia kulionya kundi la BRICS kwamba ataliwekea vikwazo na kupambana nalo kama wanachama wa kundi hilo wataendelea na juhudi zao za kutumia sarafu na fedha zao za taifa kwenye mabadilishano yao ya kibiashara na kuachana na sarafu ya dola. Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, iwapo nchi nyingine duniani zikiwemo wanachama wa BRICS zitaamua kweli kutumia fedha zao wenyewe katika miamala yao ya kibiashara na kuipiga teke sarafu ya dola, hilo litakuwa ni pigo kubwa kwa uchumi wa Marekani na pia utakuwa ni ushindi kwa madola huru duniani kama Iran na Russia ambazo zinapambana na siasa za kibeberu za kuweko kambi moja tu duniani inayoongozwa na Marekani.