Iran na Russia zahimiza kuimarishwa uhusiano wa pande mbili
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, serikali yake imedhamiria kikwelikweli kuimarisha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Russia na kukamilishwa haraka njia ya Ukanda wa Kimataifa wa Usafiri wa Kaskazini-Kusini (INSTC).
Alisema hayo jana Jumatatu alipokutana na Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Vitaly Savelyev hapa mjini Tehran.
Rais Pezeshkian amesema kuwa, serikali yake, chini ya makubaliano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, imedhamiria kutekeleza kikamilifu mradi wa reli ya Rasht-Astara ambao unaunganisha reli za Russia, Azerbaijan na Iran.
Amesema: "Iran imejitolea kikamilifu kutekeleza makubaliano hayo, na kwamba upande wa Russia nao unaweza kuanza kuchora ramani ya njia ya kufanikisha mradi huo haraka iwezekanavyo."
Vilevile amesema: Serikali ya Iran inasisitizia udharura wa kutekelezwa vipengee vyote vya makubaliano hayo na kuongeza kuwa, Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji wa Iran, Farzaneh Sadegh ndiye alipewa jukumu la kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Russia amewasilisha salamu motomoto za Rais Vladimir Putin kwa Rais Pezeshkian na amemwalika Rais wa Iran kutembelea Russia katika siku za mwanzoni mwa mwaka 2025.
Vilevile amethibitisha dhamira ya serikali ya Russia ya kutekeleza kikamilifu makubaliano ya reli ya Rasht-Astara na kuongeza kuwa, nchi yake na Azerbaijan zimekubali kujenga reli ya kisasa kwenye maeneo yao.
Ameashiria kukua usafirishaji wa mizigo kati ya Iran na Russia na kubainisha kwamba uwezo wa kubeba mizigo unatarajiwa kufikia tani milioni 15 pindi mradi wa reli ya Rasht-Astara utakapokamilika na kuanza kufanya kazi.