Iran na Saudi Arabia kuimarisha uhusiano katika sekta ya teknolojia
Rais wa Shirika la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano la Iran na Rais wa Kamati ya Mawasiliano, Anga za Mbali na Teknolojia (CST) ya Saudi Arabia katika mkutano wa pamoja huko Riyadh wamesisitiza kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA)
Mohammad Mohsen Sadr, Rais wa Shirika la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano la Iran, hivi karibuni alihudhuria Mkutano wa Usimamizi Mtandao (IGF) mjini Riyadh ambapo pembizioni mwa kikao hicho alikutana na Dr. Mohammed Al-Tamim, Rais wa Tume ya Mawasiliano, Anga za Mbali na Teknolojia (CST) ya Saudi Arabia.
Katika mkutano huu, pande hizo mbili zilionyesha hamu ya kuongeza ushirikiano katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari na kutumia uwezo ulipo.
Masuala kama vile kutumia miundombinu ya pamoja, kubadilishana uzoefu katika nyanja za majukwaa ya kitaifa ya teknolojia ya habari , kupanua ushirikiano wa posta, nyaya za intaneti zijulikanazo kama fiber optic, kufafanua mipango ya pamoja katika nyanja ya akili mnemba na hatimaye shughuli za pamoja katika sekta ya biashara zinazoinuka na zinazotegemea maarifa ya teknolojia ya habari na mifumo ya kidijitali ni baadhi ya maeneo muhimu yaliyojadiliwa katika mazungumzo hayo.
Pia katika mkutano huu kutiliwa mkazo matumizi ya uwezo na nguvu za kampuni za sekta binafsi za Iran katika miradi mikubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya Saudi Arabia.
Kulingana na ripoti hii, pande hizo mbili zilikubaliana kufuatilia masuala yaliyotajwa katika mfumo wa makubaliano ya pamoja.
Mkutano wa Usimamizi Mtandao(IGF) huandaliwa kila mwaka kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu mada zinazohusiana na usimamizi wa mtandao na Umoja wa Mataifa, ambapo wawakilishi kutoka sekta za umma, binafsi, na za kitaaluma hushiriki.