Araqchi: Kuvuka kipindi cha sasa kunahitaji kujiepusha na mifarakano
-
Sayyid Abbas Araqchi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amewaambia maafisa wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwamba: Kuvuka kipindi hiki chenye taharuki nyingi katika eneo la Magharibi mwa Asia kunahitaji busara, ushirikishwaji, ushirikiano na kuepusha mizozo na kujitakia maslahi ya muda mfupi.
Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo katika makala yake akijibu taarifa ya hivi karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria na madai kwamba Iran inaingilia matukio ya hivi karibuni nchini humo. Amesema: Matukio ya sasa nchini Syria ambayo yanafuatia kusonga mbele vikosi vya upinzani dhidi ya Bashar al-Assad vinavyoongozwa na kundi la Tahrir al-Sham, ambalo jina lake bado liko katika orodha ya makundi ya kigaidi nchini Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya na Umoja wa Mataifa, yanauweka mustakbali wa kisiasa wa Syria katika hali ya sintofahamu.

Wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika saa za mwisho za kuwepo Bashar al-Assad mjini Damascus, alifanya harakati kubwa za kuwasiliana na wenzake wa nchi za Kiarabu katika kikao cha pande kadhaa kuhusu hali ya Syria huko Doha, lakini inaonekana kwamba watawala wa sasa wa Damascus walichukua hatua za kuzidisha pengo kati ya wachezaji muhimu wa kikanda na kimataifa.
Katika siku chache zilizopita, maafisa kadhaa walioteuliwa na Abu Mohammad al-Jolani, kiongozi wa Tahrir al-Sham mjini Damascus, walitoa madai yasiyo na msingi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inajaribu kuzusha machafuko nchini Syria.