Maana ya ushirikiano mpya wa Iran na Russia kwa ulimwengu
Chombo kimoja cha habari cha Russia kimetathmini ushirikiano wa Iran na Russia na kuandika: Makubaliano ya pamoja ya kistratejia ni hatua muhimu katika kuimarika muungano kati ya mataifa haya mawili.
Katika ripoti yake, Moscow Times limechunguza makubaliano ya pamoja ya kimkakati kati ya Iran na Russia na kuandika: Iran na Russia zimeimarisha ushirikiano wao wakati huu wa mzozo wa kijiografia-kisiasa duniani, jambo ambalo linaonyesha umuhimu mkubwa zaidi wa ushirikiano huo katika miaka ijayo. Makubaliano ya pamoja ya kistratejia ambayo yanatazamiwa kuwa rasmi wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian mjini Moscow tarehe 17 mwezi huu wa Januari, ni hatua muhimu katika kuimarisha muungano huo kati ya mataifa haya mawili.

Uhusiano wa Tehran na Moscow ni zaidi ya mabadilishano ya kiuchumi, kwa sababu umekuwa ushirikiano wa kistratejia unaodhihirisha maslahi yao ya pamoja katika kuidhaminia utulivu kanda hii ya Asia Magharibi na kukabiliana na ushawishi wa Magharibi. Ushirikiano huu una taathira kubwa, hasa katika nyuga za ulinzi, biashara na nishati kwa kuzingatia kuwa nchi zote mbili zinakabiliwa na changamoto zinazofanana. Maeneo muhimu ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya usafirishaji, nishati, ulinzi na usalama wa kikanda, yatakuwa miongoni mwa makubaliano haya ya kihistoria kati ya Iran na Russia.
Dira ya kiuchumi ya Iran na Russia imechangiwa na kutegemea mauzo yao ya nje ya nishati na pia uzoefu wa nchi mbili katika kukabiliwa na vikwazo vya nchi za Magharibi. Aidha ukuaji wa ushirikiano wa nchi mbili hizi umetoa fursa ya kipekee ya kukabiliana na changamoto hizo na kufungua ukurasa mpya za ustawi wa uchumi. Moja ya nguzo kuu za ushirikiano huo ni ushoroba yaani korido ya usafirishaji ya Kaskazini-Kusini, ambao ni mradi muhimu wa miundombinu unaowezesha biashara kati ya Iran na Russia na pia washirika wao kadhaa wa kikanda na kimataifa. Uwekezaji huu wa kimkakati katika mitandao na miundo msingi ya uchukuzi, unaonyesha wazi nia ya Moscow na Tehran ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kudhamini maslahi ya pande zote katika miaka ijayo na kukabiliana barabara na vikwazo vya Magharibi.
Mbali na usafirishaji, nishati ni suala la msingi katika ushirikiano wa Iran na Russia. Nchi mbili hizi zinafanya kila ziwezalo kutafuta njia mbadala ya kukuza sekta zao za nishati licha ya vikwazo vinavyotatiza kufikia kwenye masoko ya nchi za Magharibi. Tukiachana na mafuta na gesi, Iran na Russia zinafanya bidii ya kuboresha uchumi wao kwa kupata masoko mapya barani Asia (hasa huko India) ili kupunguza utegemezi wao kwa masoko ya Magharibi kupitia kukuza ushirikiano mkubwa katika Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU).
Sifa nyingine kuu ya ushirikiano wa Iran na Russia ni ushirikiano wao wa kijeshi. Russia na Iran zimekuwa zikijidhaminia pakubwa silaha hasa katika teknolojia ya kisasa ya kijeshi kama vile ndege zisizo na rubani (droni).

Wakati huo huo, inatazamiwa kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Iran na Russia huenda ukaimarishwa kwa kutilia mkazo jitihada za pande zote za kukabiliana na ugaidi, kuhakikisha usalama wa kanda hii na kushirikiana pakubwa katika biashara ya silaha. Suala hili litakuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha usalama wa nchi zote mbili na uwezo wao wa kutumia ushawishi wa kijeo-politiki katika eneo la Asia Magharibi na kwingineko.