Zarif: Moto mkali wa California unakumbusha unyama wa Israel huko Gaza
Makamu wa Rais wa Iran anayehusika na masuala ya kimkakati amelinganisha uharibifu unaosababishwa na "ghadhabu ya kimaumbile" kwa njia ya moto mkali huko California na uharibifu uliosababishwa na "unyama wa Israel" katika Ukanda wa Gaza baada ya miezi 15 ya uvamizi na mauaji ya kimbari yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi kwenye eneo hilo la Wapalestina.
Mohammad Javad Zarif, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran, ametoa mkono wa pole kwa watu wa California katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kutokana na maafa makubwa ya moto ulioathiri Los Angeles na maeneo jirani.
Zarif ameandika kuwa: "Picha za kutisha kutoka California zinakumbusha nyumba zilizoharibiwa, shule na hospitali zilizochomwa moto huko Gaza."
"Ni ubinadamu tu kuwaonea huruma watu wa California ambao wamepoteza kila kitu kwa ghadhabu ya kimaumbile, haswa kwa kuzingatia kuwa wengi wao walisimama kuonyesha mshikamano wao na watu wa Gaza ambao wamepoteza kila kitu kwa ukatili wa Israel," amesisitiza Mohammad Javad Zarif.
Tangu Jumanne iliyopita, moto mkubwa umekumba kusini mwa California na kuharibu makumi ya maelfu ya ekari za ardhi, nyumba nyingi na biashara katika eneo hilo, na ripoti za ndani zikisema watu wasiopungua 10 wamepoteza maisha hadi sasa.
Uharibifu wa kiuchumi uliosababishwa na moto mkali kusini mwa California unakadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 52 na 57.
Ujumbe huo wa Zarif umetolewa katika hali ambayo tangu Oktoba 2023 utawala wa Israel umeua Wapalestina wasiopungua 46,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 109,378 huko Gaza baada ya kuharibu na kuteketeza karibu eneo lote lililozingirwa la Ukanda wa Gaza.