Rais Pezeshkian arejea Tehran baada ya kutembelea Tajikistan na Russia
Rais Masoud Peshkeskian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikuwa kwenye ziara za kikazi za kutembelea Dushanbe na Moscow akiongoza ujumbe wa ngazi za juu kwa mwaliko rasmi wa Marais Emomali Rahmon wa Tajikistan na Vladimir Putin wa Russia, amerejea hapa Tehran mapema leo Jumamosi.
Katika ziara ya mjini Dushanbe, nchi mbili za Iran na Tajikistan zimefikia makubaliano 23 ya ushirikiano kwenye nyuga mbalimbali.
Katika safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia pia, kumetiwa saini makubaliano ya kina ya kimkakati ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akiwa ziarani nchini Russia, Rais Pezeshkian amefanya mazungumzo ya ana kwa ana kwa nyakati tofauti na Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kushiriki katika mazungumzo kati ya wajumbe wa ngazi ya juu kutoka nchi hizo mbili.
Vilevile alihudhuria mkutano wa wanaharakati wa kiuchumi wa Russia na kufanya mahojiano na televisheni ya taifa ya nchi hiyo.
Dk Pezzeshkian amesema: "Ushirikiano kati ya Iran na Russia ni mafanikio, na kadiri ushirikiano huo unavyoimarika ndivyo adui anavyozidi kukata tamaa ya kuweza kufanikisha njama zake za kuvuruga amani na usalama kwenye eneo hili."
Rais wa Iran amesisitiza kuwa: "Serikali mbili za Iran na Russia zimeazimia kwelikweli kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Moja ya sababu muhimu zinazolifanya suala hilo kuwa na udharura mkubwa ni kwamba nchi hizi mbili ni jirani na zina mambo mengi yanayofanana. Kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo za mawasiliano na usafirishaji ni muhimu sana.