Kutekelezwa Makubaliano ya Kifedha kati ya Iran na Russia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121688-kutekelezwa_makubaliano_ya_kifedha_kati_ya_iran_na_russia
Gavana wa Benki Kuu ya Iran, Mohammadreza Farzin, amesema kuwa kupitia utekelezaji wa makubaliano ya kifedha kati ya Iran na Russia, sarafu za mataifa haya mawili zitakuwa msingi wa biashara kati ya nchi hizo kwa mujibu wa kiwango cha mabadilishano kilichokubaliwa sokoni.
(last modified 2025-01-21T02:33:07+00:00 )
Jan 21, 2025 02:33 UTC
  • Kutekelezwa Makubaliano ya Kifedha kati ya Iran na Russia

Gavana wa Benki Kuu ya Iran, Mohammadreza Farzin, amesema kuwa kupitia utekelezaji wa makubaliano ya kifedha kati ya Iran na Russia, sarafu za mataifa haya mawili zitakuwa msingi wa biashara kati ya nchi hizo kwa mujibu wa kiwango cha mabadilishano kilichokubaliwa sokoni.

Farzin amesisitiza kuwa utekelezaji wa makubaliano haya utamaliza changamoto zote za kifedha na kibenki katika biashara kati ya Iran na Russia. Pia amesema kuwa sarafu za kidijitali za Iran na Russia zitahusishwa katika miamala ya kiuchumi. 

Kwa mujibu wa makubaliano haya, hati ya utekelezaji wa hatua za pamoja kati ya benki kuu za Iran na Russia  imejikita katika maeneo matatu makuu: 

1. Matumizi ya sarafu za kitaifa katika biashara kati ya nchi hizi mbili.

2. Kuwezesha miungano ya mifumo ya mawasiliano ya benki za nchi hizi, inayojulikana kama Sepam na SPFS. 

3. Kuwezesha muunganiko wa mitandao ya malipo ya kadi za benki za nchi hizi. 

Farzin amebainisha kuwa kufuatia makubaliano haya ya kifedha, miamala itafanywa kwa kutumia sarafu za ndani, yaani Riali na Ruble, na wala hakuna haja ya kutumia sarafu nyingine. Hatua hii ni mwanzo wa kuimarisha biashara na kupunguza hatari za kubadilisha sarafu nyinginezo. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya VTB ya Russia ambayo ni benki ya pili kwa ukubwa nchini humo, biashara kati ya Iran na Russia iliongezeka kwa asilimia 30 katika miezi tisa ya mwaka 2023 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa kuna ongezeko la matumizi ya sarafu za kitaifa katika biashara ya nje. 

Kutekelezwa kwa makubaliano ya kifedha kati ya Iran na Russia ni hatua muhimu katika kupambana na sarafu ya dola ya Kimarekani, ambayo mara nyingi hutumiwa na Marekani kama chombo cha kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi. Utekelezaji huu pia unalenga kuimarisha ushirikiano wa kifedha kati ya mataifa hayo, hasa ikizingatiwa kuwa Iran na Russia ni wanachama wa kundi la BRICS, ambalo linaweka mkazo kwenye maendeleo ya biashara kwa misingi ya makubaliano ya pande mbili. 

Katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na kuongezeka kwa vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, suala la kutumia sarafu nyingine badala ya dola limepewa uzito mkubwa na mataifa mbalimbali ulimwenguni. Mataifa hayo yamekuwa yakikosoa matumizi ya dola kama chombo cha mashinikizo na kujaribu kupunguza kuitegemea kwa njia mbalimbali. 

Sera ya kuondoa dola na kutumia sarafu za kitaifa imekuwa muhimu hasa kwa mataifa yanayokabiliwa na vikwazo vya Marekani. Wanachama wa BRICS, ikiwa ni pamoja na Russia na China, wamekuwa wakifanya biashara zao kwa kutumia sarafu zao. Kwa mfano, biashara kati ya China na Russia sasa inafanywa kwa kutumia Yuan na Ruble. 

Benki ya Dunia iliripoti kuwa sehemu ya dola katika akiba za fedha za kigeni duniani imekuwa ikipungua. Kwa ushirikiano wa kimataifa, nafasi ya dola kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi inazidi kupungua, jambo ambalo limewapelekea viongozi wa Marekani kuingiwa na wasiwasi. 

Hata ingawa Rais ajaye wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuweka ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa kutoka nchi za BRICS ikiwa zitaanzisha sarafu mbadala, mwenendo wa sasa unaonyesha ongezeko la matumizi ya sarafu za kitaifa na kupungua kwa nafasi ya sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kifedha.