Pezeshkian: Iran na Russia hazitakubali kuburuzwa na maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121868-pezeshkian_iran_na_russia_hazitakubali_kuburuzwa_na_maadui
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, mapatano kamili ya ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Russia yanaonyesha kwamba Tehran na Moscow kamwe hazitakubali matakwa ya kupindukia ya maadui, akisisitiza kuwa nchi mbili hizi zitashirikiana kuunda sera zinazotoa kipaumbele kwa masuala ya utulivu, usalama, maendeleo na ustawi wa uchumi katika eneo.
(last modified 2025-01-25T03:03:41+00:00 )
Jan 25, 2025 03:03 UTC
  • Pezeshkian: Iran na Russia hazitakubali kuburuzwa na maadui

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa, mapatano kamili ya ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Russia yanaonyesha kwamba Tehran na Moscow kamwe hazitakubali matakwa ya kupindukia ya maadui, akisisitiza kuwa nchi mbili hizi zitashirikiana kuunda sera zinazotoa kipaumbele kwa masuala ya utulivu, usalama, maendeleo na ustawi wa uchumi katika eneo.

Rais Pezeshkian aliyasema hayo wakati wa mahojiano na kituo cha runinga cha 'Channel 1' cha Russia jana Ijumaa, ambapo amesisitiza umuhimu wa kusainiwa kwa mapatano ya kimkakati ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, pamoja na mipango ya Iran na Russia ya kuzidisha na kupanua ushirikiano wao.

Amesema makubaliano hayo kati ya Iran na Russia yanashughulikia mazungumzo ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kupiga jeki ushirikiano katika nyanja za reli, barabara, biashara, nishati na umeme.

Akijibu swali kuhusu uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi na Marekani au Israel dhidi ya Iran, au iwapo Russia  itashambuliwa na nchi nyingine, Rais wa Iran amesema, "Tumeazimia kutoshirikiana na mvamizi kwa njia yoyote ile, na hatutaruhusu shambulio kama hilo kutokea.”

Rais Pezeshkian wa Iran (kulia) akipokewa na mwenzake wa Russia

Kwingineko katika matamshi yake, Pezeshkian amelaani vikali jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na Lebanon, kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na Ulaya.

Amesema, "Hakuna mfumo au sheria ya kimataifa inayoruhusu nchi yoyote kupiga mabomu na kuwaua watu wasio na hatia, hata wakati wa vita, lakini Wazayuni wanafanya hivyo kwa urahisi."