Iran yamhutubu Trump: Mashinikizo mengine ya juu, kushindwa tena US
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesisitiza kuwa, duru mpya ya kutekeleza sera ya "mashinikizo ya juu" ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu itapelekea kushindwa tena Washington.
Araghchi amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri leo Jumatano hapa Tehran na kuongeza kuwa, "Sera ya mashinikizo ya juu zaidi tayari imeonekana kushindwa, na jaribio lolote la kuifufua itasababisha kushindwa tena (Marekani)."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran alikuwa akizungumzia sera ambayo Marekani ilipasisha wakati wa muhula wa kwanza wa Donald Trump, baada ya Washington kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015, na kuweka vikwazo zaidi na vya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinyume cha sheria.
Siku ya Jumanne, Trump aliendeleza hatua mpya "kali" zinazolenga, eti "kuzuia" Iran kuunda "silaha ya nyuklia." Trump pia ametia saini amri ya utendaji, inayoidhinisha hatua 'kali zaidi' dhidi ya Iran, huku akidai kuwa, "(Wairani) Hawawezi kuwa na silaha ya nyuklia, tutakuwa wagumu sana ikiwa watasisitiza kufanya hivyo."
Akijibu bwabwaja hizo za Trump, Araghchi amesema, "Ikiwa suala kuu ni kwamba Iran haipaswi kufuatilia silaha za nyuklia, hili linaweza kufikiwa na sio jambo gumu."
"Msimamo wa Iran uko wazi, na ni mwanachama wa NPT (Mkataba wa Kuzuia Utengenezaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia), na pia kuna fatwa (amri ya kidini) ya Kiongozi Muadhamu, ambayo imetufafanulia suala hilo," ameongeza.