Rais Pezeshkian: Iran itazima njama zote za maadui
(last modified Mon, 10 Feb 2025 11:27:25 GMT )
Feb 10, 2025 11:27 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran itazima njama zote za maadui

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian anasema Jamhuri ya Kiislamu itafanya juu chini kuzima njama zote zinazopangwa na maadui dhidi ya taifa hili.

Rais wa Iran ameyasema hayo leo Jumatatu alipokuwa akihutubia umati mkubwa wa watu katika maadhimisho ya mwaka wa 46 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 mjini Tehran, ambapo amekosoa madai ya hivi majuzi ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba anataka kufanya mazungumzo na Iran.

Amesema haingii akilini Trump anataka mazungumzo na Iran na wakati huo huo anapasisha amri ya kiutendaji ambayo inaiagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kutekeleza kampeni yenye lengo la "kufanya mauzo ya mafuta ya Iran kufikia sifuri."

"Trump anasema tufanye mazungumzo, halafu ... anatia saini na kutangaza njama zote zinazowezekana za kuyapigisha magoti Mapinduzi [ya Kiislamu]," Rais Pezeshkian ameeleza.

Rais Pezeshkian amebainisha kuwa, Trump anadai kuwa Iran inavuruga usalama wa eneo lakini "ni Israel ambayo, kwa kuungwa mkono na Marekani, ndiyo chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo kwa namna inavyowashambulia kwa mabomu watu wanaodhulumiwa wa Gaza, Lebanon, Palestina, Syria, Iran na popote inapotaka."

Rais wa Iran akihutubia umati mkubwa wa Wairani katika Medani ya Azadi, Tehran

Rais wa Iran ameongeza kuwa, Rais wa Marekani anadai kupignia amani na utulivu, lakini ukweli wa mambo ni kuwa anamtetea mhalifu ambaye amehukumiwa na taasisi za kimataifa, akimrejelea waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Pezeshkian ametahadharisha kwamba, maadui na watu wenye nia mbaya na taifa hili wanataka kuzusha mifarakano nchini Iran. "Hata hivyo," anaendelea kusema, "hawatambui kwamba, chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na kwa kuwepo daima na kujitolea mhanga kwa watu [wa Iran], (maadui) wataenda makaburini na ndoto zao hizo."