Iran yawasilisha malalamiko Baraza la Usalama la UN kuhusu vitisho vya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122598-iran_yawasilisha_malalamiko_baraza_la_usalama_la_un_kuhusu_vitisho_vya_trump
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayehusika na Masuala ya Kisheria na Kimataifa amesema Iran imewasilisha malalamiko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2025-02-11T11:16:36+00:00 )
Feb 11, 2025 11:16 UTC
  • Iran yawasilisha malalamiko Baraza la Usalama la UN kuhusu vitisho vya Trump

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayehusika na Masuala ya Kisheria na Kimataifa amesema Iran imewasilisha malalamiko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kazem Gharibabadi amesema hayo leo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, siku tatu baada ya Trump kusema kwamba angependelea kufanya makubaliano na Iran badala ya "kuishambulia vikali... Hawataki kufa. Hakuna anayetaka kufa."

Ghraibabadi amesema ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika maandamano ya jana Jumatatu ya kuadhimisha mwaka wa 46 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 ni "jibu kali kwa vitisho vya hivi karibuni vya Rais wa Marekani."

"Iran italinda kwa nguvu zote usalama na maslahi yake ya taifa," ameongeza Ghraibabadi.

Ameongeza kuwa, Tehran "itafuatilia kisheria" matamshi ya Trump ambayo "yanakwenda kinyume na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa," na kubainisha kuwa barua ya malalamiko itasajiliwa kama hati rasmi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akijibu matamshi ya Trump katika hotuba yake ya jana kwenye sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Pezeshkian alitahadharisha kwamba, "maadui na watu wenye nia mbaya na taifa la Iran wanataka kuzusha mifarakano nchini Iran hata hivyo, hawatambui kwamba, chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na kwa kuwepo daima na kujitolea mhanga kwa watu [wa Iran], (maadui) wataenda makaburini na ndoto zao hizo."