Tehran yalaani tishio la Trump la kutumia mabavu dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122628-tehran_yalaani_tishio_la_trump_la_kutumia_mabavu_dhidi_ya_iran
Iran imelaani vikali tishio la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo na kusema linatia wasiwasi mkubwa na linaonyesha kutowajibika ipasavyo.
(last modified 2025-02-12T03:16:20+00:00 )
Feb 12, 2025 03:16 UTC
  • Amir Saeid Iravani
    Amir Saeid Iravani

Iran imelaani vikali tishio la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo na kusema linatia wasiwasi mkubwa na linaonyesha kutowajibika ipasavyo.

Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama.

Amir Saeid Iravani amesema matamshi ya kizembe na kichochezi ya Trump yanakiuka waziwazi sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

"Kutokana na maagizo kutoka kwa Serikali yangu, ninaandika ili kuelekeza mazingatio ya Baraza la Usalama kwa matamshi ya kutisha na ya kutowajibika yaliyotolewa na Rais wa Marekani, ambapo ametishia waziwazi kutumia nguvu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema Iravani.

Ni baada ya Trump kusema katika mahojiano na vyombo vya habari yaliyochapishwa Jumamosi kwamba angependelea kufanya makubaliano na Iran badala ya "kuishambulia." "Hawataki kufa. Hakuna mtu anataka kufa," amesema Trump.

Katika taarifa nyingine ya matamshi ya kivita, wakati wa mahojiano na Fox News siku ya Jumatatu, Trump alisisitiza lugha hiyo hiyo ya vita. Alisema: "Ningependa kufanya makubaliano bila kuwalipua kwa mabomu."

Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema "kauli za kizembe na za kichochezi za Trump zinakiuka waziwazi sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, hasa Kifungu cha 2(4), ambacho kinakataza vitisho au utumiaji wa mabavu dhidi ya mataifa huru."

Mwanadiplomasia huyo wa Iran pia amelaani sera ya Trump inayoitwa "shinikizo la juu zaidi” dhidi ya Iran akiitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa kanuni na sheria za kimataifa.

Awali, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa "Wamarekani Wakitutishia tutawatishia, wakitekeleza vitisho vyao tutatekeleza vishio vyetu, na wakishambulia usalama wa taifa letu tutashambulia usalama wao bila kusita."

Imam Ali Khamenei

Ayatullah Ali Khamenei alisisitiza kuwa mwenendo huo wa kuchukua hatua sawa unatokana na Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Kiislamu na kusema: "Tunatumai kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atatujaalia taufuki katika kutekeleza majukumu yetu."