Iran yataka kuwepo uadilifu, kuheshimiana na amani ya kimataifa
(last modified Wed, 26 Feb 2025 06:41:04 GMT )
Feb 26, 2025 06:41 UTC
  • Ali Bahreini
    Ali Bahreini

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesisitiza dhamira ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuunga mkono ulimwengu wa pande kadhaa, sheria za kimataifa na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kutoa wito wa kuwepo ulimwengu unaozingatia uadilifu, heshima na amani.

Ali Bahreini ameyasema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X baada ya kikao cha ngazi ya juu cha Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Ameandika kuwa: "Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa UN mjini Geneva, tunathibitisha dhamira yetu thabiti ya kuwepo ulimwengu wa kambi kadhaa, kuheshimu sheria za kimataifa na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa." 

Amesema: "Tunapokaribia maadhimisho ya miaka 80 ya kutiwa saini mkataba huu, njooni tuendeleze ulimwengu ambamo ndani yake uadilifu, heshima na amani vitashinda ukandamizaji na migawanyiko."

Mkutano wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa unafanyika wakati taasisi za kimataifa zikikabiliwa na changamoto nyingi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za baadhi ya nchi.

Iran ikiwa mwanachama wa kundi hilo daima imekuwa ikitilia mkazo ulazima wa kukabiliana na hatua za baadhi ya wahusika wa kimataifa za kujichulia maamuzi ya upande mmoja na kudhoofishwa taasisi za kimataifa.