Waziri wa Mambo ya Nje: Iran itajibu barua ya Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu itajibu barua ya Rais wa Marekani Donald Trump katika siku zijazo kupitia njia zinazofaa.
Araghchi ametoa maelezo hayo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha moja kwa moja katika Kanali ya Pili ya Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) siku ya Alhamisi.
Pia, Araghchi amebainisha kuwa hatua ya kidiplomasia kutoka kwa Wamarekani, iinajumuisha barua ambayo ina ombi la mazungumzo.
Amesisitiza kuwa sera ya Jamhuri ya Kiislamu ni wazi: "Hatutashiriki mazungumzo ya moja kwa moja chini ya mashinikizo, vitisho, au vikwazo vilivyoongezeka."
Kwa mujibu wa Araghchi, mazungumzo lazima yafanyike kwa usawa na chini ya hali za haki.
Waziri wa mambo ya nje pia amesema kuwa barua hiyo inatisha zaidi, lakini pia inadai kuwa kuna fursa.
Kuhusu barua hiyo, amesema Jamhuri ya Kiislamu itazingatia vipengele vyote vya barua hiyo.
"Tunashughulikia kila kipengele cha barua kwa kina, tunazingatia kila kitu kwa undani na kwa umakini," amesema.
"Tutachunguza vipengele vya vitisho na fursa," Araghchi alisema, akinukuu Kamanda wa kupambana na ugaidi wa Iran, shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, akisema, "Ndani ya kila tishio, pia kuna fursa."
Mnamo mwanzoni mwa Machi, rais Donald Trump alisema kwamba alikuwa amemuandikia barua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei.
Mwezi Februari, Ayatullah Khamenei, katika mkutano na maafisa wa Jeshi la Anga jijini Tehran, alisema kuwa uzoefu umeonyesha kuwa mazungumzo na Marekani hayasaidii kutatua matatizo ya Iran.