Iran: Ulimwengu wa Kiislamu una wajibu wa kukomesha jinai za Israel Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i124250-iran_ulimwengu_wa_kiislamu_una_wajibu_wa_kukomesha_jinai_za_israel_ghaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali ukatili wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza na kusisitizia udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka na za moja kwa moja za nchi za Kiislamu za kukomesha jinai hizo.
(last modified 2025-03-22T23:18:44+00:00 )
Mar 22, 2025 23:18 UTC
  • Iran: Ulimwengu wa Kiislamu una wajibu wa kukomesha jinai za Israel Ghaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali ukatili wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza na kusisitizia udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka na za moja kwa moja za nchi za Kiislamu za kukomesha jinai hizo.

Sayyid Abbas Araghchi ametoa mwito huo katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan jana Jumamosi na kuzitaka nchi za Kiislamu duniani kote kufanya juhudi kubwa na za pamoja kukabiliana na uvamizi wa Israel.

Araghchi ametoa mwito huo baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha wimbi jipya la jinai na mauaji ya umati huko Gaza tangu siku ya Jumanne ikiwa ni kukanyaga moja kwa moja makubaliano ya HAMAS na Israel ya kusitisha mapigano kwenye ukanda huo.

Wimbi hilo jipya la mauaji ya umati yanayoifanywa na utawala wa Kizayuni limeshapelekea zaidi ya Wapalestina 1,000 kuuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Idadi hiyo inaingia kwenye takriban Wapalestina 48,000 waliouliwa shahidi kikatili na Israel katika kipindi cha zaidi ya miezi 15 ya mashambulizi yake ya kinyama huko Ghaza.

Jinai hizo zinaendelea huku waziri wa vita wa Israel anayeitwa Israel Katz akitishia kuendelea na jinai zao hizo na kupora baadhi ya maeneo ya Ghaza kama Hamas haitawaachia huru mateka wa Kizayuni waliobakia katika ardhi ya Palestina suala ambalo ni kinyume kabisa na mapatano ya kusimamisha vita. HAMAS wamesema, wataendelea kusimama imara katika Muqawama wao wa haki na wameitaka dunia kutoiacha peke yake katika kukabiliana na ukatili huo wa kuchupa mipaka wa Israel.