Siku ya Quds; Taliban: Imam Khomeini alifikisha kilio cha Wapalestina kwa walimwengu
Naibu kaimu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Taliban mjini Herat amesema kuwa, kubuniwa Siku ya Kimataifa ya Quds na Imam Khomeini (MA) kumepelekea kufika kwa walimwengu kilio cha Wapalestina wanaodhulumiwa kila upande na kudhihirisha umoja wa umma wa Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Rahmatullah Faizan, Naibu Kaimu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Taliban huko Herat, amesema hayo na kusisitizia ulazima wa kuchukuliwa hatua dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni. Amesema: "Tuko katika mkesha wa Wiki ya Kimataifa ya Quds, wiki ambayo iliasisiwa miaka 45 iliyopita na kiongozi wa Kiislamu Ayatullah Khomeini ili kufikisha kilio cha Wapalestina kwa walimwengu na kuonyesha umoja wa umma wa Kiislamu dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni."
Ameongeza kuwa: Hatua za Ayatullah Khomeini zimekuwa na nafasi muhimu katika kuuamsha umma wa Kiislamu na kuimarisha moyo wa Muqawama, lakini ushindi wa haki katika vita hivyo vya kutisha hautapatikana isipokuwa kwa kujitolea mhanga na kuchukua hatua za kivitendo. Lakini inasikitisha Waislamu wengi wanakataa kujitolea muhanga katika njia hiyo ya haki.
Faizan aliendelea kusema: "Leo, ukombozi wa Quds Tukufu si tu ni wajibu wa kidini, bali pia ni ujumbe wa kihistoria na wa kibinadamu ambao hautafikiwa bila ya kugharamika na bila ya kujitoa mhanga."
Amesema: Kimya cha umma wa taifa la Kiislamu mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni ni usaliti usiosameheka, na wakati Waislamu duniani kote wakiadhimisha Siku ya Quds, Quds Tukufu inaendelea kupondwa chini ya ukandamizaji na umwagaji damu wa kutisha wa Uzayuni wa kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, ili kuifanya kadhia ya Palestina iwe hai daima na milele, Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo maandamano hufanyika dunia nzima kutangaza uungaji mkono wa Quds na kadhia nzima ya Palestina.