Iran inajiundia asilimia 90 ya zana zake za kivita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i124324-iran_inajiundia_asilimia_90_ya_zana_zake_za_kivita
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda vya Kieletroniki Iran (IEI) amesema kuwa uwezo wa  kijeshi na kiulinzi wa Iran unategemea wataalamu wa ndani ya nchi.
(last modified 2025-03-25T02:35:15+00:00 )
Mar 25, 2025 02:35 UTC
  • Iran inajiundia asilimia 90 ya zana zake za kivita

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda vya Kieletroniki Iran (IEI) amesema kuwa uwezo wa  kijeshi na kiulinzi wa Iran unategemea wataalamu wa ndani ya nchi.

Akizungumza na IRNA Jumapili, Brigedia Jenerali Amir Rastegari amesema Iran kwa sasa ina uwezo wa kutengeneza vifaa vya kujihami katika nyanja mbalimbali.

Afisa huyo wa kijeshi amesema: "Katika sekta ya ulinzi, zaidi ya asilimia 90 ya vifaa na mifumo iliyopo ya Jeshi letu lenye nguvu imeundwa na kutengenezwa kabisa na mashirika ya viwanda vya Wizara ya Ulinzi na mashirika mengine tanzu."

Amebaini kuwa Shirika la Viwanda vya Kieletroniki la Iran linatengeneza zana za kijeshi katika sekta za anga, nchi kavu na baharini ikiwa ni pamoja na meli za kivita.  Ameendelea kusema kuwa: "Hadi sasa, zaidi ya mifumo 7,000 ya ulinzi imeundwa katika nyanja mbalimbali na kukabidhiwa Jeshi."

Aidha amesema leo Iran  inamiliki meli za kivita za kisasa kabisa ambazo zimeundwa kikamilifu na wataalamu wa ndani ya nchi. Brigedia Jenerali Rastegari amebaini kuwa wataalamu wa Iran wamefanikiwa katika kubuni vifaa, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya mawasiliano, rada, vita vya kielektroniki na mifumo ya sonar.

Ameongeza kuwa meli ya kivita ya Iran inayojulikana kama Dena, imeundwa kikamilifu ndani ya nchi na, ilikabidhiwa Jeshi la Wanamaji la Iran mwaka 2022 na hadi sasa imesafiri duniani kote, ikiwa imesafiri katika masafa ya zaidi ya kilomita 55,000 katika bahari tano za dunia.

Mafisa wa Iran mara kwa mara wamesisitiza kuwa nchi hii haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na nguvu zake za makombora, ambazo zinakusudiwa kuimarisha ulinzi, na kwamba haitafanya mazungumzo yoyote kuhusu kupunguza uwezo wake wa ulinzi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei mara kwa mara amesisitiza umuhimu wa kudumisha na kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Iran, huku akiwakosoa maadui kwa kuhoji uwezo wa Iran katika sekta ya makombora ya kujihami.