Iran: Hakuna mazungumzo yatakayofanyika chini ya mashinikizo, lazima Marekani ibadilishe siasa zake
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa haitashiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani chini ya mashinikizo ya 'vikwazo vya juu zaidi' na vitisho.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ambaye ameongeza kuwa, "maadamu hakuna mabadiliko makubwa yanayoonekana katika mtazamo wa upande wa pili kuhusu watu wa Iran, siasa zetu zitaendelea kuwa wazi na zisizobadilika."
Araghchi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran Jumatatu alipoelezea msimamo wa Iran kuhusu kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.
Ameongeza kwamba kwa sasa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja yaliyoko katika ajenda ya Iran kwani Marekani inaituhumu Iran kila siku. Pamoja na hayo, Araghchi amesisitiza kuwa, “hata hivyo, njia ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja inabaki kuwa wazi."
Araghchi amebainisha kwamba Iran haitapoteza fursa yoyote katika kulinda maslahi yake ya kitaifa. Rais Donald Trump wa Marekani alisema katika mahojiano na Fox News mapema mwezi Machi kwamba alimtumia barua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, ambapo alisema ameionya Iran kwamba ima ianzishe mazungumzo kuhusu makubaliano ya nyuklia au ikabiliwe na hujuma ya kijeshi.
Kauli hiyo ilifuatiwa na vikwazo vipya dhidi ya Iran ikiwa ni katika kutekeleza sera ya Trump inayoitwa 'Mashinikizo ya Juu Zaidi' dhidi ya Iran.
Iran imesema haitashiriki katika mazungumzo na Marekani iwapo mazungumzo kama hayo yataandamana na mashinikizo na vitisho. Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya wa Hijria Shamshia mnamo 21 Machi, Ayatullah Khamenei aliitahadharisha Marekani kuhusu kutumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran. Kiongozi Muadhamu alisema Marekani inapaswa kujua kwamba katika kuamiliana na Iran, hawawezi kufika popote kwa kutumia vitisho.