Iran imevuka 'mistari myekundu' ya Magharibi katika teknolojia ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125054-iran_imevuka_'mistari_myekundu'_ya_magharibi_katika_teknolojia_ya_nyuklia
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami, amesisitiza uwezo wa ndani wa Iran  katika sayansi ya nyuklia, akieleza kuwa mataifa ya Magharibi yameshindwa kuinyima Jamhuri ya Kiislamu teknolojia hiyo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 11, 2025 22:49 UTC
  • Iran imevuka 'mistari myekundu' ya Magharibi katika teknolojia ya nyuklia

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami, amesisitiza uwezo wa ndani wa Iran  katika sayansi ya nyuklia, akieleza kuwa mataifa ya Magharibi yameshindwa kuinyima Jamhuri ya Kiislamu teknolojia hiyo.

Akizungumza wakati wa sala ya Ijumaa jijini Tehran, Eslami ameeleza kuwa nchi za Magharibi zinataka kuhodhi teknolojia ya nyuklia kwa kutumia upendeleo na vikwazo vya kisiasa, huku zikikataa kustahimili maendeleo ya programu ya nyuklia ya Iran.

Amesema: “Jambo muhimu ni kuwa tumevuka 'mistari myekundu' waliyojiwekea kiholela na kinyume cha sheria katika uga wa nishati ya nyuklia.

Eslami ameongeza kuwa teknolojia ya nyuklia sasa si tu uwezo wa kisayansi, bali imekuwa sehemu ya urithi wa kitaifa — rasilimali ya kimkakati iliyokita mizizi kwenye fikra na dhamira ya watu wa Iran, ikiendelea kukua na kusonga mbele.

Halikdhalika amesisitiza kuwa mataifa ya Magharibi "hayawezi kukubali uwepo wa taifa huru kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, linalosimama sambamba nao katika majukwaa ya kimataifa."

Eslami aidha amebaini kuwa juhudi zote za mataifa ya Magharibi za kuzuia maendeleo ya Iran zimegonga mwamba. Amesema: “Kwa rehema za Mwenyezi Mungu, hawajapata mafanikio yoyote kupitia hujuma au upinzani wao, na hawatfanikiwa kamwe."

Katika muktadha wa kiteknolojia, Eslami amesema kuwa zaidi ya mataifa 30 duniani yanaonesha nia ya kununua bidhaa za nyuklia kutoka Iran , hii ikiwa ni ishara ya uhalisia wa uwezo wa teknolojia ya nyuklia nchini.

Aidha, amekosoa vikali nafasi ya Marekani katika kuzuwia Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuhimiza matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia duniani.

kuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami

Amefichua kuwa: “Iran ndiyo nchi iliyopitia idadi kubwa zaidi ya ukaguzi wa IAEA kuliko nchi nyingine yoyote."

Licha ya hali hiyo, bado kuna madai kutoka kwa mataifa ya Magharibi kwamba Iran haikubali ufuatiliaji na inaendeleza shughuli za nyuklia kwa siri ,  madai ambayo Eslami aliyapuuza kama propaganda isiyo na msingi.

Katika miaka ya karibuni, kila mara Iran ilipokaribia kufikia makubaliano ya ujenzi wa mitambo ya nyuklia na mataifa ya kigeni, mashinikizo kutoka kwa Magharibi yamewalazimu wawekezaji kujiondoa kwenye miradi hiyo. Amehitimisha kwa kusema: "Pamoja na vikwazo vya Marekani na vizuizi vya Magharibi, tumefanikisha mafanikio makubwa katika programu yetu ya nishati ya nyuklia ya amani."