Iraq: Tuna hamu ya kushirikiana na Iran kuimarisha utulivu wa kieneo
Rais wa Iraq, Abdul Latif Rashid ametangaza utayarifu wa nchi yake wa kufanya kazi na kushirikiana na Iran ili kuhakikisha kuwa eneo hili la Asia Magharibi linakuwa na utulivu na usalama.
Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian jana Ijumaa, Rais Rashid alitoa hakikisho kwamba serikali na taifa la Iraq daima litashirikiana na kusimama upande wa Iran.
"Wananchi na serikali ya Iraq daima wamekuwa wakiwatakia mema majirani na marafiki zake nchini Iran," ameeleza bayana Rais wa Iraq.
Kwa upande wake, Rais Masoud Pezeshkian amesema kukuza uhusiano baina ya Iran na nchi jirani ya Iraq ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu.
Pezeshkian amebainisha kuwa, "Uhusiano wa Iran na Iraq ni moja ya maeneo muhimu zaidi ya sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na tunawatazama watu wa nchi rafiki na jirani ya Iraq kama ndugu zetu."
Kadhalika Rais wa Iran amesema anatumai fursa itapatikana hivi karibuni kwa mkutano wa ana kwa ana na mwenzake wa Iraq, ili kuwawezesha viongozi hao wawili kujadili njia za kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa pande mbili.
Rais Abdul Latif Rashid wa Iraq pia amesema ana hamu ya kufanya mkutano wa uso kwa uso na Dakta Pezeshkian ili kujadili fursa za kuimarisha zaidi ushirikiano wa mataifa haya mawili jirani.