Iran yalaani shambulizi la kinyama dhidi ya raia wa Pakistan
Ubalozi wa Jamhur ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan umelaani shambulio la woga dhidi ya kundi la raia wa Pakistan katika mkoa wa Sistan- Baluchistan.
Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Islamabad umelaani vikali shambulio la woga lililolenga raia wa Kipakistan katika mkoa wa Sistan-Baluchistan nchini Iran, na kusisitiza kuwa wahalifu, wanashirikiana na ugaidi wa kimataifa kwa lengo la kuvuruga amani na usalama katika kanda hii.
Idara ya Diplomasia ya Umma na Habari katika ubalozi wa Iran mjini Islamabad leo Jumapili imetoa taarifa na kutangaza kuwa: Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu unalaani vikali shambulio la kinyama na la woga la kutumia silaha dhidi ya raia wanane wa Pakistan katika mkoa wa Sistan - Baluchestan nchini Iran.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Ugaidi ni janga sugu na tishio la pamoja katika kanda nzima na wahalifu wamekusudia kuvuruga amani katika kanda hii kwa kushirikiana na ugaidi wa kimataifa.
Taarifa hiyo imesema: Nchi zote zinapasa kufanya juhudi kwa pamoja ili kutokomeza aina zote za ugaidi na misimamo mikali ambayo imegharimu maisha ya maelfu ya watu ajinabi katika miongo ya karibuni.