Taratibu ambazo Iran inaona zinahitajika ili kurekebisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125242-taratibu_ambazo_iran_inaona_zinahitajika_ili_kurekebisha_mkataba_wa_umoja_wa_mataifa
Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Masuala ya Kisheria na Masuala ya Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amewasilisha mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa wajumbe wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa katika kikao cha tatu cha Waratibu wa Kitaifa wa Hati ya Marafiki wa Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa na Moscow.
(last modified 2025-04-16T06:19:43+00:00 )
Apr 16, 2025 06:19 UTC
  • Taratibu ambazo Iran inaona zinahitajika ili kurekebisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa

Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Masuala ya Kisheria na Masuala ya Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amewasilisha mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa wajumbe wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa katika kikao cha tatu cha Waratibu wa Kitaifa wa Hati ya Marafiki wa Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa na Moscow.

Katika kikao hicho, Gharibabadi amesisitizia kuundwa kamati ya kisheria kuchunguza ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuwasilisha ripoti za kumbukumbu kuhusu suala hilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amependekeza katika kikao hicho kujumuishwa kwenye vipaumbele vya kazi za Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa mambo yafuatayo: Kupigania uhuru wa nchi na kuundwa sheria za kuzuia uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine, wajibu wa kuchukuliwa hatua kali za kisheria za kupinga vitendo vya upande mmoja vya kutwisha mambo yake sambamba na kukuza fikra ya kuweko maamuzi ya pamoja ya pande zote ya kukabiliana na njama za maamuzi ya upande mmoja tu. 

Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Masuala ya Kisheria na ya Kimataifa, ametoa mwito pia wa kutangulizwa mbele juhudi za kuleta utatuzi wa kidiplomasia wa mizozo na migogoro ya kimataifa, kufanyika mageuzi ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa hasa Baraza la Usalama, na kutiwa nguvu suala la kuheshimiwa sheria na haki za kimataifa.

Umoja wa Mataifa

 

Sehemu nyingine ya mapendekezo ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika kikao hicho ni pamoja na kuimarishwa ushirikiano wa pande nyingi, hasa kutokana na ushirikiano huo kuwa katika hali dhaifu mno hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Amesema, taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimeshindwa kutekeleza majukumu yao kudumisha amani na kulinda usalama wa kimataifa. 

Vilevile ameelezea masikitiko makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu hali mbaya ya Ghaza na kuongeza kuwa: "Vyombo vya kivita vya utawala ghasibu wa Israel vinawalenga kimakusudi raia na miundombinu muhimu ikiwemo hospitali, magari ya kubebea wagonjwa, wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu na hata waandishi wa habari."

Kundi la Marafiki wa Umoja wa Mataifa ni taasisi ndani ya Umoja wa Mataifa ambayo ilianzishwa mjini New York mwezi Julai 2021. Mkutano wa tatu wa waratibu wa kitaifa wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulioandaliwa na Moscow, una ajenda kama vile kutafuta mbinu zinazofaa za kupambana na maamuzi ya upande mmoja na kuchunguza maafa yanayosababishwa na ukoloni wa kimataifa sambamba na kuimarisha ushirikiano ndani ya kundi hilo.

Matamshi ya Gharibabadi katika kikao cha tatu cha Waratibu wa Kitaifa wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa yanadhihirisha vipaumbele vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuleta amani na uadilifu kimataifa. Matukio yanayotokea leo hii hususan huko Ghaza yanaonesha kuwa, jamii ya kimataifa inahitaji kuwa na utaratibu tofauti na wa huko nyuma kama kweli inataka kulinda haki za wanyonge na kukabiliana na dhulma na jinai za wavamizi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Umoja wa Mataifa uliundwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Umoja huo uliundwa kwa mujibu wa hali na mazingira ya wakati huo. Miaka mingi sana imepita tangu wakati huo. Ni wazi kabisa kwamba jumuiya hiyo inahitaji kufanyiwa marekebisho ya kimsingi ili iendane na mazingira ya hivi sasa. 

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali za Marekani zimekuwa zikilitumia vibaya mara kwa mara Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu kwa ajili ya kutimiza malengo yake haramu na kuwaunga mkono washirika wa madola ya Magharibi lakini zaidi kuukingia kifua kwa hali zote, utawala wa Kizayuni wa Israel. Kukabiliana na siasa za kiistikbari za viongozi wa Marekani na kulinda haki za mataifa ya dunia ni miongoni mwa mambo muhimu sana yanayohitajika hivi sasa. 

Dira na malengo ya Iran ni kuleta marekebisho ya kiuadilifu ndani ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Suala jingine linalohimizwa na Jamhhuri ya Kiislamu ya Iran ni kukabiliana na unyanyasaji wa Marekani na nchi za Magharibi ambazo zimekuwa zikiingiza siasa kwenye mifumo ya sheria ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa katika miaka ya hivi karibuni.