Iran; mshirika wa Sudan katika kujenga upya miundombinu ya viwanda
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza udharura wa kustawisha na kuimarisha uhusiano na Sudan na kusema: Iran iko tayari kushiriki katika kujenga upya viwanda vya nchi rafiki na ndugu ya Sudan.
Muhammad Reza Aref ameyasema hayo leo, Jumatano, mjini Tehran katika mazungumzo yake na Bi Mahasen Ali Yaqoub, Waziri wa Viwanda wa Sudan. Aref amesema anatumai amani na utulivu utarejea nchini Sudan na kwamba kuanza tena shughuli za balozi za nchi mbili katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kunatoa matumaini ya kuboreka zaidi uhusiano wa pande mbili. Amesisitiza kuwa Iran iko tayari kuendeleza uhusiano na nchi rafiki na ndugu katika nyanja zote.
Makamu wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa: Wamagharibi na utawala wa Kizayuni wanachochea fitna ili kuzusha mifarakano baina ya Waislamu, kuzigawa nchi kubwa za Kiislamu na kuyawekea mashinikizo makubwa mataifa na nchi za Kiislamu lakini kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, hazitafanikiwa.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran ameshukuru kwa salamu za pole zilizotolewa na Waziri wa Viwanda wa Sudan kuhusu mlipuko wa kuhuzunisha katika Bandari ya Shahidi Rajaee hapa nchini na kuema kuwa: Mkono huo wa pole unadhihirisha kiwango cha uhusiano wa kidugu na wa karibu kati ya mataifa haya mawili rafiki na ndugu.
Uhusiano wa kistrartejia wa Jamhuri ya Kiislamu na Iran na bara kubwa na kale la Afrika umekuwa miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Iran tangu siku za awali baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran; na Iran iko katika hali nzuri ya nchi ya Sudan katika uga wa uhusiano wa kisiasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda wa Sudan ameeleza kuwa miundombinu ya nchi yake imeshambuliwa na kuharibiwa vitani na kuongeza kuwa, watu wa Sudan wameteseka sana. Ametoa wito wa kuungwa mkono na Iran ili kukabiliana na changamoto hizo.
Bi Mahasen Ali Yaqoub yupo hapa nchini kwa jaili ya kushiriki katika Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika ulioanza tarehe 27 mwezi huu na utaendelea hadi tarehe Mosi Mei.