Iran itajibu haraka uchokozi wowote wa kijeshi kutoka Marekani, Israel
Iran imelaani vikali vitisho vya karibuni kutoka Marekani na Israel kuhusiana na shambulio la kulipiza kisasi la Yemen dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), na imeahidi kulinda mamlaka na uhuru wake dhidi ya tishio lolote au matumizi ya nguvu.
Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alitoa kauli hiyo Jumatatu kupitia barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama.
Amir Saeid Iravani amesema kuwa kitendo chochote cha uchokozi wa kijeshi kutoka Marekani au kibaraka wake, utawala wa Israel, kitapokewa kwa jibu la haraka, linalolingana na la kisheria.
Aliongeza kuwa Marekani na Israel zitabeba jukumu kamili kwa madhara yote yatakayojitokeza kutokana na uchokozi huo usio halali na wa kizembe.
Iravani amesema matamshi kama hayo ya uchochezi na ya vita dhidi ya taifa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni ukiukaji mkubwa na wa wazi wa misingi ya sheria za kimataifa.
Aidha, amekemea vikali hatua ya Marekani na washirika wake ya kuifanya Bahari Nyekundu kuwa eneo la kijeshi na kufanya operesheni za kijeshi zisizo halali dhidi ya Yemen.
Baada ya shambulio la kombora la Yemen kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion katika utawala wa Israel, waziri mkuu wa utawala huo na waziri wa ulinzi wa Marekani walitaja Iran kama mhusika, wakitishia kwamba Tehran itabebeshwa dhima.
Jumatatu usiku, makumi ya ndege za kivita za Israel zilitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya malengo nchini Yemen.
Israel imetekeleza mashambulizi 50 ya anga katika mji wa bandari wa Hudaydah na kiwanda cha saruji kilichopo mashariki.
Afisa mwandamizi wa Marekani alithibitisha kwamba mashambulizi hayo ya anga yalikuwa yakitekelezwa kwa uratibu wa karibu na Marekani, mfadhili mkuu wa Israel na mshiriki katika kampeni ya kijeshi inayoendelea kwa ukatili huko Gaza.
Kituo cha televisheni cha al-Masirah cha Yemen kiliripoti kuwa Marekani ilitekeleza mashambulizi 35 tangu Mei 4 na imelenga majimbo kadhaa ya Yemen, ikiwemo al-Jawf na Marib.
Tangu Machi, Marekani, pamoja na Uingereza na Israel, zimekuwa zikitekeleza mashambulizi ya anga ya kila siku dhidi ya Yemen na zinadai kuwa zimeshambuliza zaidi ya malengo 1,000 katika taifa hilo la Kiarabu.
Tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza, vikosi vya jeshi la Yemen vimeendesha oparesheni nyingi kuunga mkono Wapalestina wanaokumbwa na vita, vikishambulia ngome za kijeshi na kiuchumi za utawala wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, pamoja na kulenga meli za Israel au meli zinazoelekea bandari za maeneo hayo yaliyokaliwa kwa mabavu.