Awamu ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani yafanyika Oman
(last modified Sun, 11 May 2025 13:03:05 GMT )
May 11, 2025 13:03 UTC
  • Awamu ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani yafanyika Oman

Awamu ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani imefanyika leo Jumapili, Mei 11, 2025 mjini Muscat kwa upatanishi wa Oman na kumshirikisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mjumbe maalumu wa rais wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Mwandishi wa shirika la habari la Mehr ameripoti kutoka Muscat, mji mkuu wa Oman kwamba, kwa mara nyingine tena mwenyeji wa duru ya nne amesimamia mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani leo Jumapili, Mei 11 mjini Muscat. Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya duru tatu za awali na mara hii yamejikita katika kujenga imani kwenye suala la nyuklia la Iran na kuondolewa vikwazo kivitendo na kwa namna inayotakiwa.

Kuhusu duru ya nne ya mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei amesema: Mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati yetu na Marekani yameanza leo mara baada ya kuwasili ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye mazungumzo hayo na baada ya Waziri wetu wa Mambo ya Nje, Sayyid Abbas Araqchi kukutana na mwenyeji wake wa Oman, Badr Al Busaidi.

Kama kawaida, mazungumzo ya leo pia yamefanyika kwa ujumbe wa Iran kuwasilisha maoni yake kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman na yeye kurejesha majibu ya mapendekezo hayo kutoka kwa ujumbe wa Marekani. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amesisitiza kuwa nchi yake ina azma ya kweli ya kutoa msaada wowote unaohitajika ili kufanikisha mazungumzo hayo.