Pezeshkian: Hatutaacha mpango wetu wa amani wa nyuklia chini ya shinikizo lolote
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Tehran kamwe haitaachana na mpango wake wa amani wa nyuklia.
Daktari Pezeshkian amesema hayo leo katika mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ambapo amesisitiza kuwa, Iran haijali mashinikizo au vitisho vinavyoikabili, akipuuzilia mbali matamshi ya uchochezi ya Rais wa Marekani Donald Trump.
"Hatutaacha kamwe mpango wetu wa amani wa nyuklia, na hata wafanye nini, hatutakubali," Pezeshkian alisema katika katika mkutano wa Jukwaa la Mazungumzo la Tehran katika mji mkuu wa Iran siku ya Jumapili.
Rais Pezeshkian alikuwa akijibu matamshi ya hivi majuzi ya Trump kwamba, Marekani lazima ihakikishe Iran haipati silaha za nyuklia huku akitishia kuanzisha mashambulizi yanayolenga mpango wa nyuklia wa Iran.
"Kama binadamu, sitakubali kulazimishwa. Haijalishi wanatushinikiza kiasi gani, nakataa kutumiwa nguvu," rais wa Iran alisema.
Mkutano wa Kimataifa wa Tehran Dialogue Forum unafanyika leo Jumapili na kesho Jumatatu, Mei 18 na 19, 2025 ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi. Wageni 200 kutoka nchi 53 duniani wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali pia wanashiriki katika mkutano huo.
Miongoni mwa washiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, jumbe kutoka nchi za Amerika ya Kaskazini, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Uturuki, Armenia, India, Japan, China, Russia, Saudi Arabia, Iraq na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, Mawaziri wa Mambo ya Nje, wawakilishi maalumu wa serikali.