Iran: Vikwazo vya Marekani ni ishara ya uhasama, diplomasia yao si ya kweli
Iran imelaani vikali msururu wa vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani, ikivitaja kama vitendo vya uadui dhidi ya watu wa Iran na ushahidi kuwa madai ya Marekani kuhusu kutafuta suluhisho la kidiplomasia ni ya kinafiki.
Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema kuwa kila kifurushi kipya cha vikwazo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na kinazidi kuwabebesha viongozi wa Marekani mzigo wa maamuzi yenye madhara kwa watu wa kawaida.
Aidha, ameongeza kuwa hili “linathibitisha kuwa Wamarekani wana mtazamo wa uhasama dhidi ya wananchi wa Iran, na kwamba hakuna mtu anayepaswa kuamini madai yao ya kuwa na nia ya dhati katika diplomasia.”
Amesisitiza kuwa Marekani haina dhamira ya kweli katika masuala yoyote, jambo linaloongeza ugumu katika mazungumzo yanayoendelea.
Kwa mara nyingine ameeleza msimamo wa Iran wa kusisitiza njia ya mazungumzo ya kidiplomasia, akisema kuwa Iran haina cha kuficha: “Mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani. Mwelekeo huu unaonyesha umakini wetu katika mazungumzo.”
Msemaji huyo wa Iran amesisitiza kuwa kuendelea kwa vikwazo vya Marekani hakutabadilisha dhamira ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali kutaibua maswali kuhusu nia ya kweli ya Marekani katika mchakato huu.
Iran imeshawahi kueleza mara kadhaa kuwa vikwazo vya Marekani havina athari kubwa kwa uchumi wake. Hata hivyo, viongozi wameonya kuwa kuweka vikwazo wakati mazungumzo ya nyuklia yakiendelea kunaweza kuathiri imani ya Tehran katika mchakato huo wa mazungumzo.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yalianza mapema mwezi Aprili chini ya upatanishi wa Oman. Tangu wakati huo, pande hizo mbili zimefanya duru nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuondolewa kwa vikwazo.
Pande zote mbili zimeelezea mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kama yenye mwelekeo chanya kwa ujumla.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya hivi karibuni ya mjumbe wa kikanda wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff, aliyedai kuwa Washington haitaruhusu Iran kuwa na hata asilimia moja ya uwezo wa kurutubisha madini ya urani, Bw. Baghaei alisema: “Suala la urutubishaji ni sehemu ya mzunguko wa kawaida wa sekta ya nyuklia ya Iran na haliko mezani kujadiliwa.”
Amesisitiza kuwa teknolojia ya urutubishaji ya Iran ni muhimu ili kuhakikisha kuwa sekta ya nyuklia ya nchi hiyo inaendelea bila kukwama.
“Urutubishaji ni haki ya kisheria ya Iran na tumeeleza bayana msimamo wetu,” amesema.
Amewakosoa maafisa wa Marekani kwa kutoa matamko yanayokinzana mara tu wanaporudi nyumbani baada ya kila duru ya mazungumzo, na kusema kuwa wanapaswa kueleza wazi iwapo wana nia ya kweli katika mazungumzo hayo au la.