Rais Pezeshkian: Hakuna nchi inayoweza kuipigisha magoti Iran yenye umoja
-
Rais Masoud Pezeshkian
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa hakuna nchi inayoweza kuwapigisha magoti wananchi wa Iran na hakuna kizuizi chochote kinachoweza kukwamisha ustawi wao madhali wanadumisha umoja na mshikamano wao.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika katika mji wa Zanjan leo Alkhamisi, Pezeshkian amepongeza ulinzi madhubuti na wa kuenziwa wa watu wa Iran, polisi na askari usalama, pamoja na wataalamu wa makombora wakati wa vita vya kivamizi vya siku 12 vya Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mwezi Juni mwaka huu.
Rais wa Iran amesifu juhudu kubwa za vikosi vya ulinzi vya Iran likiwemo Jeshi la Taifa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wakati wa vita vya kutwishwa.
Amesisitiza kuwa taifa la Iran na vikosi vyake vya ulinzi vililinda umoja wa ardhi nzima ya nchi hii licha ya kukabiliwa na vikwazo vikali.
"Licha ya vitisho na mashinikizo yote ya maadui, vikosi vya majeshi yetu viliushinda utawala wa Kizayuni ambao ulikuwa umejizatiti kwa silaha na mfumo wake wa ulinzi wa anga wa Iron Dome na Marekani," amesema Rais Pezeshkian.