Maspika wa Mabunge ya Iran na Tanzania wataka kuimarisha ushirikiano wa Kibunge
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge ya Dunia (IPU).
Mohamed Baqir Qalibaf amesema katika mazungumzo yake na Dkt. Ackson Tulia kwamba, inatarajiwa kuwa masuala yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu yazingatiwe na kupewa umuhimu katika mikutano ya kimataifa.
Spika wa Bunge la Iran amesema, leo tunaona kile kinachotokea huko Gaza kinasikitisha. Kwa bahati mbaya, watoto, maeneo yasiyokaliwa na watu, na hata kambi ya Msalaba Mwekundu wanalengwa na kushambuliwa na Wazayuni. Wanatumia maji na chakula kama silaha za vita.
Akizungumzia umuhimu wa kustawishwa uhusiano kati ya Iran na Tanzania, Galibaf amesema: "nyanja za nishati, kilimo, teknolojia, sayansi na taaluma zina uwezo mzuri wa kukuza uhusiano wa pande mbili. Katika suala hili, kumefikiwa maelewano mazuri ambayo tuko tayari kuyatekeleza."
Kwa upande wake Tulia Ackson, rais wa Umoja wa Mabunge Dunia (IPU) ametoa salamu za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi kwa wananchi na makamanda wa Iran katika uvamizi wa hivi karibuni wa Israel, akisema: "Serikali za nchi hizo mbili zina maingiliano mazuri, hivyo tunapaswa pia kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya mabunge."
Akieleza kuwa wanafunzi wa Kitanzania wanasoma nchini Iran na kwamba maingiliano ya kisayansi kati ya nchi hizo mbili yako katika kiwango kizuri, Spika wa Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania aliongeza: "Pia kuna mipango katika nyanja ya kilimo ambayo Tanzania inaweza kunufaika hasa kwa kuzingatia na uzoefu wa Iran."