Marekani inafutilia nini katika kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran?
Marekani imeweka vikwazo vipya ili kuzuia uuzaji nje wa mafuta ya Iran.
Siku ya Jumanne, ikiwa ni katika muendelezo wa mashinikizo ya juu zaidi ya Washington dhidi ya Tehran, Wizara ya Hazina ya Marekani iliyawekea vikwazo makampuni 7 na meli 9 za mafuta kwa kisingizio cha kuwa na nafasi katika mauzo ya mafuta ya Tehran na kukwepa vikwazo dhidi ya Iran.
Wizara hiyo imedai kwamba hatua hiyo imechukuliwa katika fremu ya vikwazo vilivyowekwa Julai 3 mwaka huu na Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Wizara ya Hazina ya Marekani (OFAC), ambavyo vililenga mtandao wa Salim Ahmed Saeed. Kwa mujibu wa Wamarekani, mtandao huu unasafirisha mafuta mchanganyiko ya Iraq na Iran na hivyo kuipa mapato makubwa serikali ya Iran.
Tarehe 4 Februari mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini hati ya kuendeleza sera ya mashinikizo ya juu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakati huo huo kudai kuwa yuko tayari kuzungumza na Rais wa Iran. Hata hivyo, licha ya kufanyika kwa duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na kudai kutumia diplomasia kuhusiana na Tehran, lakini Juni 13, wakati duru ya sita ya mazungumzo hayo ilikuwa imepangwa kufanyika Juni 15, maeneo ya Tehran na baadhi ya miji mingine, ikiwa ni pamoja na vituo vyake vya nyuklia, yalilengwa kwa mashambulizi ya kijeshi, ambapo idadi kubwa ya wanasayansi, makamanda wa ngazi za juu na raia wa kwaida waliuawa.
Pia, tarehe 22 Juni, Marekani yenyewe ilishambulia vituo vya nyuklia vya Fardo, Natanz na Isfahan, ambapo vikosi vya jeshi a Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilijibu hujuma hizo za kijeshi. Hatua hiyo ya kichokozi ya Washington ilithibitisha wazi hatua zisizo halali za Marekani katika kushambulia nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa bila ya idhini ya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na vile vile kwenda kinyume na kanuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na Mkataba wa NPT.
Sasa, ikiwa ni katika kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran na baada ya kufanyika shambulio hilo la kijeshi, utawala wa Trump unajaribu kutekeleza mashinikizo hayo kwa kupunguza au kusimamisha kabisa mauzo ya mafuta ya Iran kupitia vikwazo vya aina hiyo vinavyotangazwa mara kwa mara. Ni wazi kuwa, lengo kuu la Marekani ni kuongeza mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kupunguza rasilimali zake za kifedha. Hatua hiyo ni sehemu ya stratijia ya "mashinikizo ya juu kabisa" ambayo inalenga kubadilisha mienendo ya Iran katika nyanja tofauti ukiwemo mpango wake wa nyuklia, kuunga mkono makundi ya mapambano ya ukombozi na makombora yake ya kujilinda.

Malengo makuu ya vikwazo vipya vya Marekani ni:
-Kupunguza mapato ya mafuta ya Iran kwa lengo la kupunguza uwezo wa kifedha wa serikali wa kugharamia mipango ya vikosi vyake vya kijeshi na kiusalama.
-Kuvuruga mtandao wa mauzo ya mafuta ya Iran: Marekani imeyawekea vikwazo mashirika, meli na watu wanaohusishwa na "mtandao" wa uuzaji mafuta ya Iran ili kuzuia njia zisizo rasmi za usafirishaji wa mafuta.
-Kuzuia kukwepwa vikwazo: Mashirika mengi yaliyowekewa vikwazo yako katika nchi za tatu kama vile Uchina, UAE, Ugiriki na Visiwa vya Marshall, ambayo Washington inadai yanaisaidia Iran kukwepa vikwazo.
-Kudhoofisha diplomasia ya nishati ya Iran: Kwa kupunguza ufikiaji wa Iran katika masoko ya mafuta ya kimataifa, Marekani inajaribu kupunguza ushawishi wa Iran kieneo na kimataifa.
-Kuongeza mashinikizo ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia: Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa vikwazo hivi vinaweza kuilazimisha Iran kukubali makubaliano mapya kuhusu mpango wake wa nyuklia, ingawa Iran imesimamisha mazungumzo kwa muda huu kutokana na Marekani kukiuka makubaliano hayo.
Radiamali ya Iran kuhusu vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya mauzo ya mafuta yake nje ya nchi
Jibu la Iran kwa kawaida huwa ni mchanganyiko wa misimamo ya kisiasa, hatua za kidiplomasia na juhudi za kupunguza athari za kiuchumi za vikwazo. Kuhusu vikwazo vya hivi karibuni vya mafuta, Iran imechukua misimamo ya pande kadhaa, ambayo inaweza kufupishwa ifuatavyo:
Misimamo rasmi:
-Kulaaniwa vikwazo: Viongozi wa Iran, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, wamevichukulia vikwazo hivyo vipya kuwa "haramu" na "ukiukwaji wa sheria za kimataifa," na kusisitiza kuwa hatua hizo hazitaathiri matakwa ya Iran.
-Kuendeleza njia ya muqawama: Iran imetangaza kuwa, itaendeleza siasa zake katika uga wa mauzo ya mafuta na ustawi wa kiuchumi na kuwa haivichukulii vikwazo hivyo kuwa kizingiti kikubwa.
Hatua za vitendo:
-Kuongeza ushirikiano na washirika wa Asia: Kuhusu suala hili, Iran imejaribu kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na nchi kama vile Uchina, India na Russia ili kupunguza sehemu ya mashinikizo yanayotokana na vikwazo.
-Kutumia mbinu mbadala za kuuza mafuta, ikiwa ni pamoja na matumizi ya makampuni ya kati, kubadilisha njia za usafiri na kuuza mafuta papo kwa hapo au kwa sarafu isiyo ya dola.
-Kuongeza maingiliano na nchi jirani na kambi zinazopinga vikwazo: Iran inajaribu kupanua ushirikiano wake wa kiuchumi na kisiasa na nchi zinazopinga siasa za vikwazo za Marekani, ikiwemo na baadhi ya wanachama wa BRICS.
Kadhalika, katika baadhi ya sehemu, Iran imewasilisha malalamiko yake katika taasisi kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ili kuhoji uhalali wa vikwazo hivyo vya kidhalimu.