Marais wa Iran na Misri wahimiza umoja dhidi ya uvamizi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130672-marais_wa_iran_na_misri_wahimiza_umoja_dhidi_ya_uvamizi_wa_israel
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Doha yanadhihirisha kutozingatiwa kanuni na mifumo ya kimataifa.
(last modified 2025-09-11T07:23:59+00:00 )
Sep 11, 2025 07:23 UTC
  • Marais wa Iran na Misri wahimiza umoja dhidi ya uvamizi wa Israel

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Doha yanadhihirisha kutozingatiwa kanuni na mifumo ya kimataifa.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran na mwenzake wa Misri  Abdel Fattah al Sisi wamelaani mashambulizi ya jinai ya utawala wa Israel dhid ya Qatar na kuutolea wito Ulimwengu wa Kiislamu kudhihirisha msimamo wa umoja na madhubuti dhidi ya hujuma ya Israel. 

Marais wa Iran na Misri wameeleza haya katika mazungumzo ya simu jana Jumatano. 

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Iran amesema kuwa wakati wowote inapotaka, Israel inatekeleza mashambulizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya nchi mbalimbali bila kusita. 

Siku ya Jumanne, ndege za kivita za Israel zilitekeleza mashambulizi katika mji mkuu wa Qatar, Doha lengo likiwa ni kuwauwa viongozi wa harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambao walikuwa wamekutana huko Doha kujadili pendekezo la karibuni la Marekani kwa ajili ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza. 

Rais Pezeshkian ameyatolea wito mataifa ya Kiislamu kuzuia vitendo zaidi vya kinyama dhidi ya nchi za Kiislamu. Aidha amempongeza rais al Sisi wa Misri kwa kulaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Qatar.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Misri amelaani vikali mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar na akasema Misri inapinga pakubwa mashambulizi yoyote dhidi ya ardhi za Kiislamu au kukiukwa mistari myekundu ya Ulimwengu wa Kiislamu.