Iran yalaani uingiliaji wa Marekani katika masuala yasiyoihusu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130898-iran_yalaani_uingiliaji_wa_marekani_katika_masuala_yasiyoihusu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa kauli kali ya kulaani unafiki, hadaa na uadui wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kisingizio cha kumbukumbu ya machafuko ya Shahrivar mwaka 1401 Hijria Shambia na kusema kuwa huo mfano wa wazi wa uingiliaji wa masuala ya Iran ambayo hayaihusu Marekani ndewe wala sikio.
(last modified 2025-09-17T06:47:08+00:00 )
Sep 17, 2025 06:47 UTC
  • Iran yalaani uingiliaji wa Marekani katika masuala yasiyoihusu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa kauli kali ya kulaani unafiki, hadaa na uadui wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kisingizio cha kumbukumbu ya machafuko ya Shahrivar mwaka 1401 Hijria Shambia na kusema kuwa huo mfano wa wazi wa uingiliaji wa masuala ya Iran ambayo hayaihusu Marekani ndewe wala sikio.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa Tehran inaichukulia kauli iliyojaa unafiki, hadaa na uadui ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kisingizio cha kumbukumbu ya mwaka wa machafuko ya Shahrivar 1401 kuwa ni mfano wa wazi wa jinai na uingiliaji wa mambo ya ndani ya Iran unaofanywa na Marekani katika masuala yasiyoihusu kivyovyote vile na inalaani uingiliaji huo wa kibeberu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imesema: Hakuna Muirani mwenye akili timamu na mzalendo anayeweza kuzubaishwa na kulaghaiwa na madai ya kinafiki ya Marekani ya kujifanya ni rafiki mwenye huruma hasa kwa kuzingatia kuwa tawala zote za Marekani zina historia ndefu ya kuingilia masuala ya Iran na kufanya jinai mbalimbali dhidi ya Wairani - kuanzia mapinduzi ya aibu ya 1953 hadi kushirikiana na Saddam katika vita vya 1980-1988 mpaka kuiunga mkono serikali ya Saddam katika kutumia sumu za kemikali dhidi ya wananchi wa Iran miaka ya 1980-1988.

Aidha mwaka 1988 Marekani ilitungua kwa makusudi ndege ya abiria ya Iran na hadi sasa inaliwekea taifa hili vikwazo vya kikatili na imeshirikiana na utawala wa Kizayuni kushambulia vituo vya nyuklia na kuua wanasayansi wa Iran, maafisa wa SEPAH, pamoja na wanawake na watoto wadogo wakati wa shambulio la kijinai la mwezi Juni mwaka huu.