Pezeshkian: Maadui wanajaribu kuzuia maendeleo ya taifa kupitia vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135206-pezeshkian_maadui_wanajaribu_kuzuia_maendeleo_ya_taifa_kupitia_vikwazo
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali mashinikizo ya nchi ajinabi dhidi ya taifa la Iran.
(last modified 2026-01-07T04:27:18+00:00 )
Jan 07, 2026 04:27 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian
    Rais Masoud Pezeshkian

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali mashinikizo ya nchi ajinabi dhidi ya taifa la Iran.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tehran jana Jumanne, Rais Masoud Pezeshkian alisema kuwa maadui wa Iran wanajaribu kuzuia maendeleo ya nchi hii kupitia vikwazo vya kiuchumi huku wakijidhihirisha kama watetezi wa wananchi wa Iran.

Pezeshkian amesema: Wale wote waliofanya jinai na mauaji ya halaiki sasa wanadai kuwa watetezi wa haki za binadamu. Ametaja hatua hiyo kuwa yenye kukinzana. 

Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika Tehran, Rais wa Iran aliashiria pia migogoro ya binadamu na kukiukwa pakubwa haki za binadamu huko Gaza, Lebanon na Palestina.

Amesema, wanawake, watoto na wazee na raia wengine wanalengwa kiholela kwa mashambulizi ya mabomu, na bado wahusika wanazungumzia haki za binadamu. Haya ni maafa halisi. 

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa chanzo halisi cha nguvu na utajiri wa Iran kiko kwa watu wake. Amesisitiza kuwa taasisi zote za uongozi zikiwemo za utawala, Bunge, halmashauri na vyombo vingine lazima viendelee kuwa na uhusiano wa karibu na wananchi.

"Ombi langu pekee ni kwa Iran kujifakharisha na watu wake waishi kwa heshima," amesema Pezeshkian. 

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais wa Iran ameangazia umuhimu wa kufanyika mazungumzo na kuwa huru kujieleza na akatilia mkazo msisitizo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa kuanzisha vikao vya majadiliano ya wazi katika vyuo vikuu.

Ameongeza kuwa wanafunzi ni mali ya taifa, na watu ndio mtaji mkuu wa nchi. Wajibu wa serikali ni kuwasikiliza wananchi na kutatua matatizo yao.