Pezeshkian: Waliofanya fujo na machafuko Iran si wananchi; ni magaidi kutoka nje
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, adui amewaingiza Iran magaidi waliopewa mafunzo maalumu ya kigaidi ili kufanikisha malengo yake na kwamba waliofanya fujo, machafuko na uharibifu katika kona mbalimbali za Iran, si katika wananchi waliokuwa wanaandamana.
Rais Pezeshkian alisema hayo jana Jumapili wakati alipozungumza na wananchi kwa njia ya televisheni na kusema: Adui amewaingiza humu nchini magaidi waliopata mafunzo maalumu lengo likiwa ni kushadidisha machafuko na ukosefu wa amani nchini.
Amesema kwamba jukumu la serikali ni kutatua matatizo na kundoa wasiwasi wa wananchi; na zaidi ya hilo serikali ina wajibu wa kutotoa mwanya kwa wafanya machafuko kuivuruga nchi; na kwamba familia zisiwaruhusu vijana wao kujiingiza katika ghasia za magaidi hao. Rais Pezeshkian ameeleza haya ikiwa ni majibu yake kuhusu matukio ya hivi karibuni ya machafuko humu nchini.
Vilevile ameashiria maandamanao ya siku za karibuni ya wafanyabiashara na kuongeza kuwa: Katika kikao na pande mbili hizo kati ya Serikali na wafanyabiashara, serikali imesikiliza daghadagha na malalamiko yao na imeshaanza kuchukua hatua za kutatua changamoto hizo. Kwenye kikao hicho baina ya serikali na wafanyabiashara kulichukuliwa maamuzi muhimu ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya tabaka hilo katika jamii. Hii ni kwa sababu serikali inataka kutatua matatizo yao kadiri inavyowezekana.
Aidha Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa, adui katika vita vya siku 12 pia alikusudia kuitumbukiza Iran katika machafukoni na kwamba maadui wa wananchi wa Iran hii leo pia wameazimia kushadidisha vurugu ili wapate mwanya wa kuingilia zaidi masuala ya ndani ya nchi hii.