Iran yasema imeongeza nguvu ya makombora yake tangu vita na Israel
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran amesema kuwa Iran sasa ina makombora bora na imara zaidi kuliko yale yaliyotumika wakati wa vita vifupi kati yake na utawala wa Kizayuni Israel mwaka uliopita.
Brigedia Jenerali Reza Talaei-Nik amesema Jumamosi kwamba Iran pia imeongeza idadi ya makombora yake tangu kumalizika kwa vita hivyo vya mwezi Juni.
Alinukuliwa na shirika la habari la Tasnim akisema, “Uwezo wa Iran katika nguvu ya makombora, kwa wingi na kwa ubora, umeongezeka ikilinganishwa na vita vya siku 12 vya kulazimishwa, na uwezo wa ulinzi wa makombora wa nchi umeimarika na kuwa madhubuti zaidi kutokana na uzoefu uliopatikana wakati wa vita.”
Jenerali huyo ameongeza kuwa Iran imeendeleza uwezo wa hali ya juu wa makombora ili kukabiliana na vitisho vipya, huku akisisitiza kwamba maendeleo hayo yataendelea kuwekwa siri ili kumshangaza adui wakati muafaka utakapowadia.
Alipuuzilia mbali vitisho vya hivi karibuni vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, akisema kuwa lugha ya kusuasua ya maadui inaonyesha wazi hofu yao kuhusu uwezo wa ulinzi wa Iran na nguvu ya makombora yake.
Makombora ya Iran yaliyotumika katika vita dhidi ya Israel yalisababisha uharibifu mkubwa kwa utawala huo, yakipiga malengo mengi ya kijeshi na kiuchumi katika maeneo yanayokaliwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Wataalamu wa kijeshi wanaamini kuwa athari inayoongezeka ya makombora ya Iran yaliyolenga maeneo ya Israel ilikuwa sababu muhimu iliyomlazimu Marekani kushinikiza utawala huo kukubali kusitisha mapigano tarehe 24 Juni.
Maafisa wa Iran na makamanda wa kijeshi wameonya kuwa nchi haitasita kutumia nguvu zake kubwa za makombora dhidi ya malengo yanayohusishwa na Marekani katika eneo la Asia Magharibi endapo Washington itaamua kuishambulia Iran.