Iran: Tutatoa jibu la 'kujutisha' kwa uchokozi wowote wa maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135928-iran_tutatoa_jibu_la_'kujutisha'_kwa_uchokozi_wowote_wa_maadui
Iran imeonya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itatoa "jibu la kujutisha" kwa kitendo chochote cha uchokozi, ikisisitiza kwamba taifa hili sasa lina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi kuliko hapo awali.
(last modified 2026-01-26T12:19:16+00:00 )
Jan 26, 2026 12:19 UTC
  • Iran: Tutatoa jibu la 'kujutisha' kwa uchokozi wowote wa maadui

Iran imeonya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itatoa "jibu la kujutisha" kwa kitendo chochote cha uchokozi, ikisisitiza kwamba taifa hili sasa lina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi kuliko hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake wa kila wiki hapa mjini Tehran leo Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ameashiria vitendo vya hivi karibuni vya Marekani katika eneo na kufanyika kwa mazoezi ya kijeshi na kubainisha kuwa, "Tutatoa jibu la 'kuzuia' kwa uchokozi wowote wa maadui."

"Tumekabiliana, na tunaendelea kukabiliana na aina zote za vita mseto. Kufuatia uchokozi wa Juni, katika miezi michache iliyopita, tumekabiliwa na vitisho vipya kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni," amesema.

Mamlaka za Iran zimethibitisha kwamba, mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel yalihusika moja kwa moja, yakitoa ufadhili, mafunzo, na usaidizi wa vyombo vya habari kwa wafanya fujo na magaidi wenye silaha walioteka nyara maandamano ya hivi karibuni.

Baghaei amebainisha kuwa, nchi za Asia Magharibi zinafahamu kwamba, ukosefu wowote wa usalama katika eneo hili hauelekezwi dhidi ya Iran pekee, na ndiyo maana kuna wasiwasi wa pamoja miongoni mwa mataifa ya kikanda juu ya chokochoko za maajinabi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, "Iran ina imani katika uwezo wake na pia imezingatia matukio ya Juni, na itajibu uchokozi wowote kwa nguvu zaidi kuliko hapo awali kwa majibu ya kujutisha."

Kadhalika Baghaei amelaani azimio la hivi karibuni dhidi ya Iran katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, akisema limesababisha mgawanyiko katika jamii ya kimataifa. 

Kuhusu hatua ya Bunge la Ulaya kuliorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kama "shirika la kigaidi," Baghaei amesisitiza kwamba, uamuzi huo batili dhidi ya sehemu ya vikosi rasmi vya jeshi la taifa ni kinyume na sheria za kimataifa, na kwa kitendo hicho kitakuwa na matokeo mabaya.