Larijani: Asia Magharibi itatumbukia gizani US ikishambulia mtandao wa umeme wa Iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametoa onyo kali akijibu vitisho vipya vilivyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kushambulia giridi ya taifa ya umeme wa Jamhuri ya Kiislamu.
Akijibu vitisho hivyo, Ali Larijani amesema iwapo Marekani itatekeleza vitisho vyake vya kushambulia mtandao wa umeme wa Iran, basi eneo lote la Asia Magharibi litaingia kwenye kiza.
Dakta Larijani ametoa mjibizo huo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X, baada ya Trump kudai kwamba, (Wamarekani) wana uwezo wa kudumaza mtandao wa umeme wa Iran ndani ya saa moja, lakini hawajatekeleza hilo.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amejibu vitisho hivyo kwa kuandika: Iwapo watafanya hivyo, eneo lote (la Asia Magharibi) litatumbukia gizani ndani ya nusu saa, na kiza kitatoa fursa nzuri ya kuwindwa wanajeshi wa Marekani wanaokimbilia usalama wao.
Trump amedai kuwa, Washington imejizuia mpaka sasa kushambulia vituo vya kuzalisha umeme vya Iran, lakini inajiandaa kutekeleza hujuma hizo iwapo Iran itazuia usambazaji wa mafuta duniani kwa kufunga Lango-Bahari la Hormuz.
Hii ni katika hali ambayo, Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran siku ya Alkhamisi alitoa ujumbe wake wa kwanza baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, ambapo amesisitiza kuwa, wenzo wa kufunga Lango-Bahari la Hormuz unapaswa kuendelea kutumiwa.