Iran yajibu mapigo, yamtimua mwanadiplomasia wa Sweden
-
Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, sanjari na kukanusha madai ya Sweden dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, imempa mwanadiplomasia wa nchi hiyo aliyeko Tehran muda wa saa 48 kuondoka nchini, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kwa uamuzi wa Stockholm wa kukataa kumruhusu mwanadiplomasia wa Iran kuendelea na shughuli zake.
Kitengo cha Uhusiano Mwema cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kimetoa taarifa kikikanusha madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na serikali ya Stockholm dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, na kulaani uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden wa kumzuia mwanadiplomasia wa Iran anayefanya kazi katika Ubalozi wa Iran nchini humo kuendelea na majukumu yake.
Taarifa hiyo inasema: "Serikali ya Sweden, katika hatua isiyo na uhalali na inayokwenda kinyume na kanuni za sheria za kimataifa, imemtaka mwanadiplomasia anayefanya kazi katika Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Stockholm kuondoka katika ardhi ya Uswidi bila sababu yoyote ya msingi. Wakati huo huo, serikali ya Uswidi imetoa tuhuma zisizo na msingi kuhusu madai ya Iran kuingilia masuala ya usalama wa nchi hiyo."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran huku ikikanusha madai na tuhuma hizo dhidi ya Iran imeeleza kuwa, hatua ya serikali ya Sweden ya kuzuia shughuli za mwanadiplomasia huyo wa Iran haina uhalali wowote na inailaani vikali.
Hatua hii ya serikali ya Sweden inatajwa kuwa matokeo ya ushawishi wa utawala wa Kizayuni na jaribio la kuvuruga utendaji wa kawaida wa Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Stockholm.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa itachukua hatua zinazohitajika kulinda haki na maslahi yake ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kujibu mapigo.