Araghchi: Marekani imevuruga mchakato wa mazungumzo mara kadhaa kwa kukiuka makubaliano
-
Araghchi: Marekani imevuruga mchakato wa mazungumzo mara kadhaa kwa kukiuka makubaliano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Marekani imevuruga mara kadhaa michakato ya kidiplomasia kwa kukiuka makubaliano na kutumia nguvu. Araghchi ameyasema hayo alipokutana na kuufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq mjini Baghdad.
Araghchi alitembelea Baghdad kushiriki katika kikao cha 52 cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Katika mazungumzo hayo, Araghchi ameishukuru serikali na wananchi wa Iraq kwa kuandaa kwa mafanikio mkutano huo. Amesisitiza umuhimu wa kutumia kwa kiwango kikubwa zaidi uwezo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika kufuatilia masuala yanayoukabili Ulimwengu wa Kiislamu, hususan suala la Palestina, pamoja na upanuzi wa maeneo na uchochezi wa vita unaofanywa na utawala haramu wa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akizungumzia uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili jirani na za Kiislamu, amesisitiza dhamira ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuimarisha zaidi uhusiano wake na Iraq katika nyanja zote zenye maslahi ya pamoja kwa nchi hizo mbili.
Waziri Araghchi, akieleza misimamo na mitazamo ya Iran kuhusu amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi, amesisitiza kuwa, chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo hili ni ukaliaji wa ardhi za wengine na sera za kujitanua zinazofanywa na utawala wa Israel.
Amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sambamba na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, utawala huo umefanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Lebanon, Syria na Iran, hatua ambazo, kwa mujibu wa Araghchi zimehatarisha amani na usalama wa dunia.
Araghchi, akizungumzia dhamira ya Iran ya kutumia diplomasia kuzuia kuongezeka ukosefu wa usalama, alikumbusha kuwa, Marekani ndiyo iliyovuruga mara kwa mara michakato ya kidiplomasia kwa kukiuka makubaliano na kutumia nguvu. Alisema hatua hizo pia zimesababisha usafiri wa meli za kibiashara za kimataifa kukosa usalama.