Sep 07, 2016 13:20 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Saudia ikubali uchunguzi kuhusu maafa ya Mina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: "Iwapo utawala wa Saudia haupaswi kulaumiwa kuhusu maafa ya Mina, basi ukubali jopo la Kiislamu-Kimataifa lichunguze kwa karibu maafa hayo na kuweka kila kitu wazi."

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran wakati alipokutana na familia za waliokufa shahidi katika matukio ya Mina na Masjid al Haram katika msimu wa Hija mwaka jana. Amesema, uzembe na usimamizi mbovu wa ukoo wa Aal Saud katika maafa ya Mina ni jambo ambalo limethibitisha kwa mara nyingine tena, shajara hiyo khabithi na iliyolaaniwa, haistahiki kusimamia maeneo mawili matakatifu ya Waislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria kufa shahidi Mahujaji karibu elfu saba wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu katika maafa ya Mina mwaka jana na kukosoa kutochukua hatua na kutojali nchi na serikali zinginezo duniani kuhusu tukio la kusikitisha la Mina.

Kiongozi Muadhamu amesema kimya cha serikali mbali mbali na hata Maulamaa, wanaharakati wa kisiasa, wanafikra na wasomi wa Ulimwengu wa Kiislamu kuhusu kuuawa shahidi Mahujaji elfu saba wasio na hatia ni 'Balaa kubwa kwa Umma wa Kiislamu." Ameongeza kuwa, kutojali masuala kama maafa ya Mina ni msiba mkubwa na wa kweli kwa Ulimwengu wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu,  amesema hatua ya watawala wa Saudia kukataa kuomba radhi kwa maneno ni kilele cha ukhabithi na ukosefu wa heshima wa watawala hao. Amesema hata kama maafa hayo hayakufanyika kwa makusudi, ukosefu wa tadbiri,usimamizi mbovu na uzembe mkubwa ulioshuhudiwa katika utawala wa Saudia ni jinai.

Maafa ya Mina

 

Ameongeza kuwa, mtazamo mwingine wa maafa ya Mina ni kimya cha wanaodai kutetea haki za binadamu. Ameashiria kelele na propaganda za wanaodai kutetea haki za binadamu wakati baadhi ya nchi zinapotekeleza adhabu ya kifo na kusema: "Kimya kuhusu utendaji kazi mbovu wa serikali katika kutekeleza majukumu yake na kupoteza maisha wanadamu elfu saba madhulumu na wasio na hatia, ni jambo ambalo limeweka wazi utambulisho halisi wa wanaodai kutetea haki za binadamu na hivyo wale ambao wanaweka matumaini yao kwa jumuiya za kimataifa wanapaswa kupata funzo kutoka ukweli huu mchungu."

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, kuundwa jopo la kimataifa kwa ajili ya kuchunguza maafa ya Mina ni kati ya mambo ya wajibu na dharura kwa nchi za Kiislamu na wanaodai kutetea haki za binadamu. Amesema, baada ya kupita mwaka mmoja tokea kujiri tukio hilo la kusikitisha, uchunguzi wa taswira, sauti na maandishi ni jambo linaloweza, kwa kiasi kikubwa, kuweka wazi maafa hayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema waungaji mkono wa utawala wa Saudia ni washirika wake katika maafa ya Mina. Amebainisha kuwa, utawala usio na aibu wa Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, umesimama wazi dhidi ya Waislamu huko Yemen, Syria, Iraq na Bahrain na kumwaga damu ya watu wa nchi hizo. Kwa msingio huo, Marekani na waitifaki wengine wa  utawala wa Saudia ni washirika wa utawala huo katika jinai zake.

Tags