Tehran: Njama za kuharibu usalama wa Iran zimefeli
-
Mohammad Hussein Moghimi, Kaibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran
Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, njama zote za maadui za kuvuruga usalama wa Iran zimefeli.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Mohammad Hussein Moghimi akisema hayo leo mbele ya kongamano la wakuu wa wilaya na madiwani wa mkoa wa Bushehr, kusini mwa Iran na kusisitiza kuwa: Wakuu wote wa mikoa na wilaya wa Iran wametekeleza vizuri majukumu yao katika masuala ya kulinda usalama wa maeneo yao na hawakuruhusu hata hatari ndogo kuharibu usalama wa mikoa na wilaya zao.
Bw. Moghimi aidha amesema, usalama, masuala ya kijamii, maisha ya watu na masuala ya uchaguzi ni katika vipaumbele vikuu vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran na kubainisha kuwa, wizara yake ina jukumu la kulinda usalama nchini Iran na kwamba jukumu hilo ni muhimu mno hasa kwa kuzingatia hali liliyomo ndani yake hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amegusia pia uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika mwakani nchini Iran na kusema kuwa, katika uchaguzi huo sawa na chaguzi nyingine zilizopita, ni lazima haki za watu zilindwe kikamilifu kwa kutekeleza vizuri sheria, kwa utulivu kamili na bila ya kupendelea upande wowote.