Kupasishwa na Seneti ya Marekani muswada wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran
Wajumbe wa Baraza la Seneti la Marekani wamepitisha muswada wa kurefusha kwa muda wa miaka 10 mingine Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA).
Muswada wa sheria hiyo umepitishwa kwa kura 99 za wajumbe waliounga mkono bila ya kupingwa na mjumbe yeyote wa Seneti ya Marekani; na sasa unasubiri kusainiwa na Rais wa nchi hiyo Barack Obama ili uwe sheria.
Kupasishwa muswada wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran ni ushahidi mwingine wa muelekeo wa kichuki na kihasama wa Washington dhidi ya Tehran.
Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (Iran Sanctions Act) ambayo ndiyo msingi mkuu wa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996 kwa lengo la kuzuia uwekezaji mitaji mikubwa ya kigeni katika sekta ya mafuta na gesi ya Iran; na baada ya hapo ikarefushwa tena mwaka 2006 kwa kipindi kingine cha miaka 10. Sheria hiyo inamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu.
Kabla ya hapo Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha mpango huo kwa kura 419 za kuunga mkono dhidi ya kura moja tu iliyoupinga. Pamoja na hayo Ikulu ya Marekani (White House) haijaonesha msimamo maalumu kuhusu hatua ambayo Rais wa nchi hiyo Barack Obama anaweza kuchukua kuhusiana na uamuzi wa Kongresi wa kupitisha muswada huo. Msemaji wa White House Josh Earnest, alitangaza siku ya Jumatano kuwa Obama anayo mamlaka yanayohitajika kusaini vikwazo vya ziada dhidi ya Iran endapo italazimu kufanya hivyo; na kwamba kama atasaini muswada huo haitokuwa mara ya kwanza kwake kusaini miswada inayopitishwa na Kongresi ambayo haikuwa na umuhimu mkubwa.
Pamoja na hayo kwa kuzingatia kuwa Baraza la Seneti limeunga mkono kikamilifu mpango huo wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kwa kipindi cha miaka 10, hata kama Obama atatumia kura ya veto kuupinga hatoweza kuuzuia usiwe sheria. Na hasa kwa kutilia maanani kwamba hivi karibuni pia baada ya Obama kutumia kura yake ya turufu kupinga muswada wa Sheria ya Kukabiliana na Wafadhili wa Ugaidi (JASTA), Kongresi iliupitisha muswada huo kuwa sheria baada ya zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Seneti kuupigia tena kura ya "Ndiyo".
Kwa mujibu wa Katiba ya Marekani baada ya Rais kuupigia muswada kura ya veto ya kuuzuia usiwe sheria, uamuzi huo hutenguka na muswada huwa sheria endapo zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Kongresi watapiga kura tena ya kuupitisha.
Japokuwa Obama ametumia hapo kabla mamlaka yake ya amri za kiutendaji kusimamisha vikwazo vinavyohusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran baada ya kufikiwa makubaliano baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi zinazounda kundi la 5+1, lakini wajumbe wa Kongresi wanaitakidi kuwa kuna ulazima wa kupitishwa sheria hiyo kwa ajili ya kuendelea kuwa na wenzo wa mashinikizo dhidi ya Iran.
Seneta Mitch McConnell wa chama cha Republican ambaye ni kiongozi wa mrengo wa waliowengi katika Seneti ya Marekani amedai kuwa kuna ulazima wa kuendeleza vikwazo ili kuzuia kupanuka ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati. Aidha amesema kuna matumaini kuwa mnamo mwaka ujao Kongresi mpya na serikali mpya ya Marekani zitaangalia upya sera za nchi hiyo kuhusiana na Iran.
Kupasishwa mpango wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kunadhihirisha wazi jinsi Marekani isivyojali nia njema iliyoonyeshwa na Iran katika kutekeleza makubaliano ya nyuklia (JCPOA). Hivi karibuni Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alitangaza kuwa kurefushwa muda wa sheria ya vikwazo ni sawa na kupitisha na kutekeleza vikwazo vipya; na hiyo ina maana ya kukiuka waziwazi makubaliano ya nyuklia. Kwa mujibu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu endapo sheria ya vikwazo dhidi ya Iran itatekelezwa bila ya shaka utakuwa ni ukiukaji wa JCPOA na kwa msingi huo ametamka bayana kuwa Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kwa hatua hiyo.
Kwa hakika Marekani inaonesha kwamba inachotafuta zaidi ni kisingizio cha kuendeleza mashinikizo dhidi ya Iran. Licha ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, ambayo hata washirika wa Ulaya wa Washington wamekiri wazi kuwa yameondoa wasiwasi uliokuwepo kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran, lakini Marekani inataka ipatiwe majibu ya kuiridhisha pia juu ya matakwa yake mengine kama ya miradi ya makombora ya Iran, kwamba eti Iran iache kuunga mkono ugaidi, suala la haki za binadamu na pia kutaka Jamhuri ya Kiislamu iregeze msimamo wake kuhusiana na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Ni wazi kwamba Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hautotekeleza takwa lolote lile kati ya hayo kwa sababu inaitakidi kwamba ilikubali kusaini makubaliano ya nyuklia kwa ajili tu ya kuonyesha nia njema na kutatua hitilafu na tofauti zilizokuwepo juu ya suala hilo. Na ndiyo maana imeshasisitiza pia kwamba endapo ahadi na makubaliano yaliyofikiwa yatakiukwa, ikiwemo kuendelezwa vikwazo na Marekani, wakati wowote ule itakuwa na uwezo wa kuanzisha tena kikamilifu shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani.../