Iran yalaani ukatili dhidi ya Waislamu nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20800-iran_yalaani_ukatili_dhidi_ya_waislamu_nchini_myanmar
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani ubaguzi na ukatili unaofanywa dhidi ya makundi ya kidini nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2016 11:57 UTC
  • Iran yalaani ukatili dhidi ya Waislamu nchini Myanmar

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani ubaguzi na ukatili unaofanywa dhidi ya makundi ya kidini nchini Myanmar.

Bahram Qasemi ambaye alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari wa ndani na nje hapa mjini Tehran amesema kuhusu mauaji yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya kwamba, ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu hao unaielekeza jamii upande wa misimamo mikali na kwamba, kuendelea kwa mwenendo huo hakuna faida kwa upande wowote.

Waislamu wa Myanmar wanaendelea kuuawa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameashiria hatua ya Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya Iran na kusema: Marekani imedumisha tabia ya uhasama na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitakuwa mbele kukiuka makubaliano ya nyuklia na nchi za kundi la 5+1 wala kukiuka ahadi na majukumu yake. Qasemi amesema, hatua ya Baraza la Seneti la Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya Iran na yatakayofuatia baadaye ni ukiukaji wa makubaliano na wala haikubaliwi.

jengo la Baraza la Seneti la Marekani

Ameitaka Marekani kurejea katika njia sahihi na kusisitiza kuwa, Washington haina uwezo wa kushika njia tofauti na ile ya makubaliano ya pande kadhaa ya nyuklia.

Kuhusu kuundwa serikali ya uokovu wa kitaifa nchini Yemen, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, inasikitisha kwamba nchi hiyo bado ni mhanga wa mashambulizi na uvamizi wa mara kwa mara wa Saudi Arabia. Ameongeza kuwa, Tehran inakaribisha mashauriano ya kisiasa na maelewano kati ya makundi yote ya Yemen na inatarajia kuwa, mazungumzo yaliyoanza nchini humo yatapata ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nchi hiyo.