Kiongozi Muadhamu: Mapigano magharibi mwa Asia ni ya kutwishwa
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, machafuko yanayoshuhudiwa katika eneo la magharibi mwa Asia ni ya kutwishwa na ni kwa mujibu wa malengo ya kikhabithi kutoka nje.
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Rais Joko Widodo wa Indonesia ambapo sambamba na kusifu misimamo ya nchi hiyo kuhusiana na kadhia ya Palestina amesema kuwa, akthari ya migogoro inayoshuhudiwa hii leo imepandikizwa ili kuwasahaulisha watu na mgogoro mbaya zaidi katika Mashariki ya Kati na suala kuu la Ulimwengu wa Kiislamu yaani kadhia ya Palestina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameisifu shakhsia ya Ahmed Sukarno, Rais wa kwanza wa Indonesia pamoja na nafasi yake muhimu katika kuitishwa Mkutano wa Bandung ambao ulikuwa msingi mkuu wa kuanzishwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na kueleza kwamba, hii leo pia misimamo na mitazamo ya kisiasa ya Indonesia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya za kimataifa inakaribiana.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitazama Indonesia kwa jicho la udugu na ushirikiano ambapo ameashiria hatua nzuri za kimaendeleo zilizopigwa na nchi hiyo katika nyuga mbalimbali na kuongeza kwamba, Iran pia ina uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali na kwamba, taifa hili linaamini kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kufanya mambo kinyume kabisa na matakwa ya maadui na hivyo kujiweka mbali na hitilafu na mivutano baina yao.