Iran yalaani azimio la Canada dhidi yake katika Umoja wa Mataifa
Iran imelaani azimio lililopitishwa dhidi yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu.
Ghulamhussein Dehqan, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema azimio hilo kwa mara nyingine limeonyesha namna madola yanayodai kutetea haki za binaadamu yanavyohadaa walimwengu.
Siku ya Jumatatu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio ambalo lilipendekezwa na Canada dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Azimio hilo lilidai kuwa, nchini Iran kuna mateso ya wafungwa, kiwango kikubwa cha hukumu za kifo, vizingiti kwa waandamanaji, ubaguzi dhidi ya wanawake na waliowachache kidini.
Huku akipinga madai yaliyomo katika azmio hilo dhidi ya Iran, Dehqan amesema Canada yenyewe ni mkiukaji mkubwa wa haki za Wahindi wekundi ambao ni wenyeji wa nchi hiyo na pia Wacanada wenye asili ya Kiafrika. Amesema ni kichekesho kuona nchi ambazo ni wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu zikiunga mkono azimio hilo dhidi ya Iran.
Aidha amesema katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Wairani wameshiriki katika chaguzi nyingi jambo ambalo ni dhihirisho la uhuru walionao wananchi wa Iran katika kuamua na kuainisha mustakabli wa nchi yao.