AFP: Wafuasi wa dini za wachache wana usalama mkubwa nchini Iran
Shirika la habari la Ufaransa AFP limetangaza kuwa, wafuasi wa dini za wachache wakiwemo Wakristo wanaishi kwa usalama mkubwa nchini Iran na kwamba nchi hiyo ni katika nchi zenye usalama mkubwa zaidi kwa watu wa dini za wachache kwenye eneo la Mashariki ya Kati.
Shirika la habari la FARS limelinukuu shirika hilo likisema jana kuwa, jamii wa Wakristo, Mayahudi na Wazartoshti zinaishi kwa usalama mkubwa nchini Iran tangu ilipotoka amri ya Ayatullahil Udhma Ruhullah Khomeini (mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) ya kutambuliwa rasmi dini hizo nchini Iran.
Shirika hilo la habari la Ufaransa limegusia pia namna wafuasi wa dini za wachache wakiwemo Wakristo wanavyoruhusiwa kufanya ibada zao kwa uhuru kamili humu nchini na kusema, jamii ya Wakristo haikabiliwi na vizuizi vyovyote kutoka kwa viongozi wa Iran.
Mwishoni mwa ripoti yake hiyo, shirika la habari la AFP limegusia mahojiano yake na Askofu Mkuu wa Wakristo wa Iran kuhusiana na uhuru na usalama ulipo humu nchini kwa wafuasi wa dini na madhehebu zote na kusema kuwa, licha ya eneo hili kuwa kitovu cha machafuko ya kila namna, lakini Iran imekuwa na utulivu na usalama mkubwa na inapasa kusifiwa sana kwa jambo hilo.