Jan 13, 2017 14:53 UTC
  • Rouhani: Ushiriki mkubwa wa wananchi mazishi ya Rafsanjani ni alama ya umoja

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika mazishi ya Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran ni alama ya umoja na mshikamano.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo wakati alipofika katika Haram ya Imam Khomein Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo sanjari na kusoma dua na kuweka shada la maua kwenye kaburi la Ayatullah Hashemi Rafsanjani, ameomba dua kwa Mwenyezi Mungu akimtakia maghfira na rehema za Allah.

Rais Hassan Rouhani akiwa na marhum Ayatullah Hashemi Rafsanjani enzi za uhai wake

Baada ya kuzuru makaburi ya Imam Khomein na Ayatullah Hashemi Rafsanjani Rais Rouhani amezungumza na waandishi wa habari na kundi la wananchi ambapo amesisitiza kuwa, taifa la Iran litaendelea kufuata njia ya shakhsia wawili hao. Ameongeza kuwa, ushiriki mkubwa wa wananchi katika mazishi ya mwendazake Ayatullah Hashemi Rafsanjani umeonyesha umoja wa pande na makundi yote kama ambavyo pia umebainisha nafasi kubwa ya uelewa wa wananchi wa taifa hili na kwamba, makundi hayo yameudhihirishia ulimwengu kwamba Iran imeshikamana vilivyo na misingi ya mfumo wa Kiislamu.

Marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani

Akiashiria kuwa kifo cha mwanazuoni huyo ni pigo kwa wafuasi wa njia ya Imam Khomein na taifa zima la Iran Rais Rouhani amesema, katika kipindi chote cha mapinduzi na harakati za Kiislamu, Ayatullah Hashemi Rafsanjani alivumilia mateso na matatizo mengi. Ameongeza kuwa, ushiriki wa mamilioni ya watu katika mazishi yake ilikuwa ni kutoa shukurani kwa juhudi za mwanazuoni huyo.

Ayatullah Hashemi Rafsanjani, enzi za uhai wake

Amesema kuwa, raia wa Iran hadi mwisho watakuwa kando na viongozi wao na kwamba hata baada ya kufariki dunia au kuuawa shahidi huonyesha mafungamano yao na viongozi hao.

Tags