Dec 18, 2024 02:39 UTC
  • Jumatano, 18 Disemba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 16 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria sawa na tarehe 18 Disemba 2024 Milaadia.

Miaka 1025 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mwashuhuri wa Andalusia. 

Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. 

Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania.

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa muitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria.

Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania.

Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia.

Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia. 

Otto Hahn

Tarehe 18 Disemba miaka 45 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake.

Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu.

Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu unasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.   

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, Sadeq Ganji mwambata wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lahore Pakistan alishambuliwa kwa risasi na vibaraka wa ubeberu wa kimataifa na kuuawa shahidi.

Kwa karibu miaka minne Ganji alikuwa akitekeleza jukumu lake la kutangaza na kuziarifisha thamani aali za Kiislamu na kupanua uhusiano wa kiutamaduni baina ya wananchi wa Iran na Pakistan.

Sadeq Ganji aliuawa shahidi akiwa amekaribia kurejea hapa nchini baada ya hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na wana utamaduni na shakhsia wa kielimu na kifasihi wa Lahore Pakistan. 

Sadeq Ganji