Rouhani: Uchaguzi wa Iran uliistaajabisha dunia
(last modified Sun, 06 Mar 2016 15:30:19 GMT )
Mar 06, 2016 15:30 UTC
  • Rouhani: Uchaguzi wa Iran uliistaajabisha dunia

Rais Hassan Rouhani amesema kwa mara nyingine tena kuwa wananchi wa Iran wamewastaajabisha walimwengu kutokana na namna walivyoshiriki kwa wingi katika uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wanazuoni Wataalamu uliofanyika hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari hapa jijini Tehran hii leo, Rais wa Iran amesema, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo, kulituma ujumbe duniani kuwa wananchi wa Iran wana imani na mfumo wao wa uongozi.

Rais Rouhani amesema kuwa uchaguzi huo ni wa kihistoria kutokana na kushiriki idadi kubwa ya wananchi kwenye uchaguzi huo.

Itakumbukwa kuwa, asilimia 62 ya wananchi milioni 55 waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu na wa 5 wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu uliofanyika Februari 26.

Akiashiria kuhusu athari za kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, Rais Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu imeongeza uzalishaji wa mafuta hadi mapipa milioni 1.4 kwa siku na kuongeza kwamba kiwango hicho kitaongezeka hadi mapipa bilioni 2 kwa siku kuanzia mwaka ujao wa Kiirani.

Tags